Wakaguzi wa migodi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) walisema Jumatatu kwamba wameunda kitengo cha walinzi wa maeneo ya uchimbaji madini ili kuhakikisha usalama wa usambazaji wa madini.
Uamuzi huu unakuja huku DRC, mzalishaji mkubwa wa madini ya kobalti duniani ikijaribu kuzuia magendo na ukosefu wa usalama katika sekta hiyo na kuongeza imani kwa wawekezaji.
Mpango huo utafadhiliwa na bajeti ya dola milioni 100 chini ya ubia wa kimkakati na Marekani na UAE, Shirika la Ukaguzi Mkuu wa Migodi (IGM) lilisema katika taarifa yake.
DRC, nchi ya pili kwa kuuza shaba duniani ikiwa na akiba kubwa ya lithiamu, koltan na dhahabu, inapambana na uasi katika eneo la mashariki lenye utajiri mkubwa wa madini, Uasi huo umesababisha vifo vya maelfu ya watu katika eneo hilo la nchi.
Mwaka jana Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ilitia saini mpango wa ushirikiano wa madini na Marekani ili kuimarisha ugavi na usalama.
IGM ilisema kitengo kipya cha maafisa wa usalama kitapelekwa hatua kwa hatua katika mikoa yenye DRC yenye madini na inatarajiwa kuhusisha zaidi ya wafanyakazi 20,000 ifikapo mwisho wa 2028.
Kikosi cha kwanza cha kati ya walinzi 2,500 na 3,000 kitaanza kufanya kazi kuanzia Disemba 2026, kufuatia kuajiriwa na kupitia mafunzo ya miezi sita kwa ushirikiano na jeshi.
"Nia ya Rais wa Jamhuri ni kusafisha sekta nzima ya madini, kwa kuondoa vitendo vinavyopingana na utawala bora, uwazi na ufuatiliaji wa madini," alisema Rafael Kabengele, mkaguzi mkuu wa migodi nchini.
Chini ya mpango wa ushirikiano wa madini wa Marekani na DRC, kampuni ya Virtus ilichukua majukumu ya uchimbaji madini ya shaba-kobalti ya Chemaf wakati makampuni mengine ya mataifa ya Magharibi yakionesha nia ya uwekezaji katika sekta ya madini, ikiwa ni pamoja na maeneo ya waasi ambapo ukosefu wa usalama umetatiza shughuli za awali.
Ulinzi wa sekta ya madini nchini DRC utachukua majukumu ya usalama yanayofanywa na vikosi vingine sasa hivi.
Jukumu lake litajumuisha kuhakikisha usalama katika maeneo ya migodi, kulinda shehena za madini wakati wa kusafirishwa kutoka maeneo ya uchimbaji hadi vituo vya kuchakatwa na vile vya mpakani, na kulinda uwekezaji, ilisema taarifa hiyo.
Mpango huo unatarajiwa kuimarisha imani ya wawekezaji na kuhakikisha usimamizi thabiti wa serikali katika uzalishaji madini, maafisa walisema.













