Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan, alizungumza kwa njia ya simu na mawaziri wenzake kutoka Pakistan, Afghanistan, Qatar na Saudi Arabia kuhusu mapigano ya mpakani ya hivi karibuni kati ya Pakistan na Afghanistan, ambapo wanajeshi na raia kadhaa wameuawa.
Siku ya Alhamisi, Afghanistan ilianzisha mashambulizi ya mpakani dhidi ya Pakistan kufuatia mashambulizi ya anga ya Pakistan dhidi ya Afghanistan siku ya Jumapili, yaliyosababisha vifo vya watu wengi.
Islamabad ilidai kuwa imewaua “magaidi” 70, huku maafisa wa Afghanistan na Umoja wa Mataifa wakiripoti vifo vya raia, jambo ambalo Pakistan inakanusha.
Kwa mujibu wa vyanzo vya kidiplomasia vya Uturuki, Fidan aliwapigia simu mawaziri wenzake wa Pakistan, Afghanistan, Qatar na Saudi Arabia — Ishaq Dar, Amir Khan Muttaqi, Mohammed bin Abdulrahman Al Thani na Faisal bin Farhan — siku ya Ijumaa, ili kupunguza mvutano huo.
Mazungumzo hayo yalijikita katika mapigano ya hivi karibuni kati ya Pakistan na Afghanistan.
Mvutano kati ya nchi hizo mbili uliongezeka mwezi Oktoba mwaka jana wakati vikosi vya Afghanistan viliposhambulia vituo vya mpakani vya Pakistan, siku chache baada ya Jeshi la Anga la Pakistan kufanya mashambulizi ndani ya Afghanistan.
Pakistan imekumbwa na ongezeko la matukio ya kigaidi katika miezi ya hivi karibuni, mengi yakihusishwa na kundi la Tehrik-i-Taliban Pakistan (TTP).
Pakistana inalishutumu kundi la TTP kwa kuendesha shughuli zake kutoka Afghanistan, tuhuma ambazo Kabul imekuwa ikizikanusha mara kwa mara.
Uturuki na Qatar zilichukua nafasi katika kupunguza mvutano na kufanikisha usitishaji mapigano kati ya nchi hizo mbili.
Oktoba 30, taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki ilisema kuwa mikutano ilifanyika Istanbul kwa ushiriki wa Uturuki, Qatar, Afghanistan na Pakistan, kwa lengo la kuimarisha usitishaji mapigano uliokubaliwa mjini Doha mapema mwezi huo, uliopatanishwa na Uturuki na Qatar.


















