Waziri Mkuu wa Australia amuita Muislamu aliyemnyang’anya silaha mshambuliaji "shujaa wa Australia"
Waziri Mkuu wa Australia, Anthony Albanese, amesema taifa hilo halitagawanywa na vitendo vya kigaidi, huku maelezo zaidi yakijitokeza kuhusu moja ya mashambulizi mabaya zaidi katika historia ya hivi karibuni ya nchi hiyo.
Siku ya Jumanne, Waziri Mkuu Albanese alitembelea Hospitali ya St. George kusini mwa Sydney kukutana na Ahmed Al Ahmed, Muislamu aliyemzuia mmoja wa washambuliaji wakati wa shambulio la kutisha katika ufukwe wa Bondi lililosababisha vifo vya watu 15.
Akiwa kando ya kitanda cha Al Ahmed hospitalini, Albanese alimpongeza baba huyo wa watoto wawili mwenye umri wa miaka 43 kwa ujasiri wake wa kipekee, akiielezea ujasiri huo kama alama ya umoja wa kitaifa mbele ya ugaidi.
“Ahmed, wewe ni shujaa wa Australia. Uliweka maisha yako hatarini ili kuwaokoa wengine,” Albanese aliandika baadaye kwenye mtandao wa X. “Katika nyakati mbaya zaidi, tunaona ubora wa Waustralia.”
Al Ahmed alijeruhiwa vibaya baada ya kumvamia mmoja wa washambuliaji, kumnyang’anya silaha na kuigeuza dhidi yake, hali iliyomlazimisha mshambuliaji huyo kujisalimisha. Al Ahmed alipigwa risasi mara kadhaa na kupata majeraha kwenye mkono na bega. Maafisa wa hospitali walisema hali yake iko thabiti.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya ziara hiyo, Albanese alionya dhidi ya kuruhusu hofu au chuki kuigawa nchi.
“Hivi ndivyo magaidi wanavyotaka, lakini hatutaruhusu nchi yetu igawanywe,” alisema. “Tutaungana, tutakumbatiana kama taifa, na tutavuka kipindi hiki.”
Watu 15 wauawa, 41 wajeruhiwa
Polisi wamesema shambulio hilo lilitokea Jumapili jioni kando ya ufukwe wa Bondi, ambapo mwanaume mwenye umri wa miaka 50 na mwanawe wa miaka 24 walifyatua risasi kwa umati wa watu. Watu 15 waliuawa na wengine wasiopungua 42 wamejeruhiwa na kukimbizwa katika hospitali mbalimbali jijini Sydney.
Mmoja wa washambuliaji alipigwa risasi na kuuawa papo hapo, huku mwingine akipata majeraha mabaya na kubaki chini ya ulinzi mkali, kwa mujibu wa polisi. Mamlaka zimetangaza rasmi tukio hilo kuwa ni kitendo cha kigaidi na zinaendelea kuchunguza chanzo na miunganisho inayoweza kuhusika.
Shambulio hilo limeitikisa Australia nzima, na kusababisha maombolezo na kutumwa kwa salamu za rambirambi kwa waathiriwa, pamoja na sifa kwa raia jasiri kama Al Ahmed waliojitokeza kuokoa maisha ya wengine. Bendera zilishushwa nusu mlingoti katika maeneo kadhaa ya Sydney, na mikesha ya kumbukumbu ilifanyika kando ya ufukwe Jumatatu usiku.
Maafisa walisema hatua za ziada za kiusalama zinaendelea kuchukuliwa huku taifa likiomboleza na wachunguzi wakiendelea kubaini jinsi washambuliaji walivyotekeleza shambulio hilo.