Baadhi ya matukio makubwa yaliyojiri nchini Tanzania 2025
Tanzania, mengi yametokea. Lakini haya ni baadhi tu ya mambo ambayo yameingia katika historia ya taifa hilo.
Mwaka unapoanza, watu mara nyingi hujiwekea malengo mbalimbali, lakini wakati huo huo, ili malengo hayo yatimie, baadhi huwa na tabia ya kuangalia jinsi mwaka ulivyokwisha na kutafakari baadhi ya matukio makubwa yaliyojiri.
Kwa mfano, nchini Tanzania, mengi yametokea. Lakini haya ni baadhi tu ya mambo ambayo yameingia katika historia ya taifa hilo.
Mlipuko wa ugonjwa wa Marburg Kagera
Nchi kadhaa za Afrika Mashariki ziliripoti kutokea kwa ugonjwa wa Marburg, nazo ni Rwanda, Burundi, Uganda na DRC. Tanzania nayo, kutokana na muingiliano wake na watu wa mataifa hayo, haikusalimika.
Januari 13, 2025, Shirika la Afya Duniani, lilitoa taarifa rasmi kwa nchi wanachama ya kutokea kwa mlipuko wa ugonjwa wa Marburg mkoani Kagera nchini Tanzania.
Hii ilitokana na taarifa za kuwepo kwa watu tisa walioshukiwa kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo, ikiwemo vifo vya watu wanane vilivyoripotiwa katika wilaya mbili, Biharamulo na Muleba.
Taarifa hizi zilileta taharuki nchini humo hasa katika maeneo ya mipaka, ambapo Wizara ya Afya ya nchi hiyo, ilichukuwa hatua za dharura, ikiwemo kupeleka wataalamu kusaidia kuchunguza na kutoa elimu kwa umma.
Kukamatwa kwa Tundu Lissu
Mwenyekiti wa Chama cha Upinzani Tanzania CHADEMA Tundu Lissu alikamatwa na Jeshi la Polisi, Aprili 9, 2025 akiwa Mbinga, mkoani Ruvuma. Lissu alikuwa mkoani humo katika moja ya mikutano ya Chama.
Mpaka sasa, kiongozi huyo amesalia ndani akikabiliwa na mashtaka kadhaa ikiwemo lile la uhaini. Kukamatwa kwa Tundu Lissu kumeibua hisia mbalimbali miongoni mwa wadau wa kisiasa ndani na nje ya Tanzania, ambapo wito wa kutaka serikali kumuachilia umekuwa ukitolewa mara kwa mara. CHADEMA imekuwa ikidai kuwa mashtaka dhidi ya Lissu yana mrengo wa kisiasa.
Uchaguzi Mkuu Tanzania
Lakini kubwa zaidi ni Uchaguzi Mkuu uliofanyika nchini humo Oktoba 29. Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanakiri kwamba, uchaguzi wa 2025 ulikuwa wa aina yake.
Hii ni kwa sababu, kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi nchini, taifa hilo la Afrika Mashariki lenye sifa ya ukomavu wa demokrasia na kitovu cha amani, wananchi wake walikwenda kwenye sanduku la kura, bila ushiriki wa chama kikuu cha upinzani CHADEMA. Hii ni baada ya chama hicho kususia kushiriki uchaguzi, kwa madai kwamba, kilitaka mabadiliko kwanza kabla kuingia kwenye uchaguzi.
Kauli mbiu ya CHADEMA ya "No Reform, No Election," haikuishia katika kuta zao tu, ilibebwa na baadhi ya wanaharakati walioanzisha vuguvugu mitandaoni ya kuitisha maandamano ya kudai mabadiliko na kupinga kufanyika kwa uchaguzi.
Kila kukicha, vuguvugu hilo lilionekana kuzidi kushika kasi, kiasi cha kumtoa relini aliyekuwa mgombea urais wa CCM Rais Samia Suluhu Hassan, mara kadhaa alitumia mikutano yake ya kampeni kuwatahadharisha wananchi dhidi ya kushiriki katika maandamano hayo.
Polisi nao, pamoja na viongozi wengine wa serikali waliunganisha nguvu kuwatahadharisha wananchi dhidi ya kushiriki maandamano.
Ghafla Tanzania ikawa kisiwa. Mtandao ukazimwa kwa siku kadhaa, Watanzania wakagubikwa katika giza la kutokuwa na mawasiliano. Mbali na hivyo, katika baadhi ya miji mikubwa kama vile Dar es Salaam, serikali iliweka marufuku ya watu kutotoka nje.
Baada ya siku kadhaa na hali ya utulivu kurudi, serikali ilitoa takwimu za uharibifu uliotokea ikiwemo mali za umma na watu binafsi. Hata hivyo, serikali ya nchi hiyo, bado inanyooshewa kidole cha lawama kwa kutotoa idadi kamili ya watu waliojeruhiwa na waliopoteza maisha, licha ya baadhi ya familia kuonekana kuzika vitu vya wapendwa wao baada ya kudai kukosa miili.
Hili lilikuwa ni tukio kubwa katika historia ya nchi hiyo. Kufuatia vuguru hizo, Rais wa nchi hiyo ameunda Tume ya Kuchunguza vurugu za baada ya uchaguzi, ambayo imepewa siku 90 kuwasilisha ripoti yake. Hata hivyo, ni wachache wanaoonekana kuwa na imani na Tume hiyo, kwa madai kwamba, haiko huru.
Kifo cha Jenista Mhagama
Bila shaka, jina la Jenista Mhagama sio geni katika masikio ya Watanzania. Mwanasiasa huyu ambaye alikuwa mbunge wa Peramiho kupitia chama tawala CCM, amekuwa katika siasa za nchi hiyo na kushika nyadhifa mbalimbali serikalini. Kifo chake kilichotokea Disemba 11 na kushtusha wengi.
Tanzania kuwa mwenyeji CHAN
Mwezi Agosti mwaka 2025, Tanzania pamoja na Uganda na Kenya walikuwa wenyeji wa michuano ya CHAN, na mechi ya ufunguzi ilifanyika pale jijini Dar es Salaam. Kwa ufanisi mkubwa kabisa, Tanzania ilionesha uwezo wake wa kuhodhi michuano mikubwa, ikiwa ni kipimo tosha cha maandalizi ya kuwa wenyeji kwa pamoja mashindano ya Afcon 2027.
Morocco ilishinda mashindano hayo katika fainali iliyochezwa mjini Nairobi.
Tanzania viza Marekani
Yapo mengi yaliyojiri, lakini kwa kumalizia tu, ni hatua ya hivi karibuni ya Marekani kuiorodhesha Tanzania miongoni mwa nchi ambazo zimewekwa katika Mpango wa Majaribio ya Dhamana ya Viza. Hii ikiwa na maana kwamba, Watanzania wanaotaka kwenda Marekani kwa shughuli za Kibiashara au Utalii wanatakiwa kuweka dhamana kabla ya kupewa viza.