Serikali ya Tanzania imesisitiza matumizi ya Akili Mnemba (Artificial Inteligence – AI) ikiwa ni moja ya nyenzo muhimu na ya kisasa katika kukuza mtangamano na kuharakisha maendeleo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kupitia sekta mbalimbali ikiwemo Kilimo, Elimu, Viwanda, Afya na Biashara.
Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mahmoud Thabit Kombo katika Kongamano la Nne la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu la Jumuiya ya Afrika Mashariki lililoandaliwa na Kamisheni ya Sayansi na Teknolojia ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EASTECO) kwa kushirikiana na Bazara la Vyuo Vikuu la Jumuiya ya Afrika Mashariki (IUCEA), linalofanyika jijini Kigali, Rwanda kuanzia Machi 30 hadi Aprili 1, 2026.
Waziri Kombo akizungumza katika Kongamano hilo lililowakutanisha viongozi wa ngazi za juu Serikalini kutoka nchi wanachama wa EAC, wabunifu, wanataaluma, wanadiplomasia na wadau wa maendeleo, amesisitiza nafasi ya Akili Mnemba katika kuongeza ufanisi na tija ikiwemo kuboresha utoaji wa huduma za umma na kuimarisha ushindani wa kiuchumi ndani ya Jumuiya na kwenye soko la kimataifa.
Akizungumzia mchango wa Tanzania, Waziri Kombo alieleza kuwa, Tanzania chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, imeweka kipaumbele katika kukuza sekta za Teknolojia, Uchumi wa Kidijitali na Ubunifu kama nguzo muhimu za agenda ya maendeleo ya taifa na Dira ya Maendeleo ya 2050. Alisisitiza kuwa mwelekeo huo unalenga kuchochea maendeleo jumuishi, kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuinua ustawi wa jamii hususan vijana.
Katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda, Waziri Kombo amehimiza nchi wanachama kuongeza juhudi za pamoja katika utafutaji wa rasilimali fedha za kuendesha programu mbalimbali ikiwemo utafiti na ujenzi wa miundombinu ya kidijitali, kubadilishana maarifa, kukuza ubunifu wa ndani na kuendeleza miradi ya pamoja ya teknolojia ili kujenga uthabiti wa kiuchumi na kijamii katika Jumuiya.
Mkutano huo ulifanyika chini ya kauli mbiu; “Matumizi ya Akili Mnemba kwa ajili ya Afrika Mashariki yenye Ustahimilivu, Jumuishi na Ubunifu.”
AFRIKA
2 dk kusoma
Tanzania yahimiza matumizi ya AI kuimarisha mtangamano na maendeleo EAC
Mkutano huo ulifanyika chini ya kauli mbiu; “Matumizi ya Akili Mnemba kwa ajili ya Afrika Mashariki yenye Ustahimilivu, Jumuishi na Ubunifu.”

Soma zaidi















