Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) umepanua mpango wake wa viza unapowasili kuwajumuisha raia wa Kenya na nchi nyingine tano, katika hatua inayolenga kuimarisha utalii, usafiri wa kibiashara na kuunganishwa kimataifa.
Chini ya sera hiyo mpya, iliyotangazwa na Mamlaka ya Shirikisho ya Utambulisho, Uraia, Forodha na Usalama wa Bandari ya UAE (ICP), raia wa Kenya, Afrika Kusini, Indonesia, Vietnam, Thailand na Ufilipino sasa wanastahiki kupata ‘visa-on-arrrival’ mradi watimize masharti maalum.
Huduma hiyo ambayo ilianza kutumika tarehe 25 Juni, iinaruhusu wasafiri wanaostahiki kupata viza ya siku 14 baada ya kuwasili, ambayo inaweza kuongezwa, au viza ya siku 60 baada ya kuwasili kulingana na kustahiki kwao.
Masharti maalum
Hata hivyo, mpango huo haupatikani kwa wamiliki wote wa pasipoti kutoka nchi hizo sita. Ili kustahiki wasafiri lazima pia wawe na kibali halali cha ukazi au viza iliyotolewa na Marekani, Uingereza, nchi mwanachama wa Umoja wa Ulaya, Australia, Canada, Japan, New Zealand, Singapore au Korea Kusini.
UAE ilisema upanuzi huo ni sehemu ya jitihada za kufanya usafiri kuwa rahisi zaidi, kuimarisha uhusiano wa kimataifa na kusaidia sekta zake za utalii na biashara kwa kurahisisha taratibu za kuingia kwa wageni zaidi.
Kwa wasafiri wa Kenya, tangazo hilo litarahisisha ufikiaji wa nchi ya Ghuba kwa wale ambao tayari wana viza au vibali vya ukaaji kutoka nchi zilizoteuliwa, lakini haimaanishi kuwa ‘visa-on-arrival’ bila vikwazo kwa wamiliki wote wa pasipoti wa Kenya.

















