Rais William Samoei Ruto wa Kenya anatarajiwa kuwasili nchini Tanzania kwa ziara ya kikazi ya siku mbili itakayoanza siku ya Jumatatu tarehe 4 Mei. Ziara hiyo inalenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, biashara na ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Kenya.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Ikulu ya Tanzania, akiwa nchini Rais Ruto atafanya mazungumzo rasmi na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, ambapo viongozi hao watajadili masuala mbalimbali ya ushirikiano wa kikanda na maendeleo ya kiuchumi.
Viongozi hao wanatarajiwa pia kushuhudia utiaji saini wa hati za makubaliano na mikataba ya ushirikiano.
Aidha, Rais Ruto atakutana na waandishi wa habari kwa ajili ya kutoa taarifa ya pamoja na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.
Pia anatarajiwa kushiriki Jukwaa la Biashara litakalowakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Tanzania na Kenya, kwa lengo la kuimarisha fursa za kiuchumi.
Tarehe 5 Mei 2026, Rais Ruto anatarajiwa kuhutubia Bunge la Tanzania mkoani Dodoma.





