Rais wa Taiwan Lai Ching-te alirejea nchini kwake Jumanne baada ya safari ya kushtukiza kwenda Eswatini, akisema kwamba watu wa Taiwan wana haki ya kwenda popote na hawatarudi nyuma.
China inasisitiza kuwa Taiwan ni sehemu ya eneo lake na inapinga kisiwa hicho kinachojitawala kushiriki na kujiunga katika mashirika ya kimataifa pamoja na mahusiano yake na nchi nyingine.
Lai Ching-te awali alipanga kutembelea nchi hiyo ya kusini mwa Afrika kuanzia Aprili 22 hadi 26, lakini alilazimika kufuta safari baada ya nchi kadhaa za Afrika kumnyima ruhusa ya kutumia anga zao.
China baadaye ilieleza “kuthamini sana” kwakw nchi za Afrika zilizofuta ruhusa za kutumia anga zao kwa kiongozi wa Taiwan.
Hakuna kurudi nyuma
“Hatutarudi nyuma licha ya ukandamizaji,” Lai Ching-te aliwaambia waandishi wa habari katika uwanja mkuu wa ndege wa kimataifa wa Taiwan huko Taoyuan, nje ya Taipei.
Rais Lai Ching-te aliwasili Eswatini siku ya Jumamosi, nchi pekee yenye uhusiano wa kidiplomasia na Taiwan barani Afrika, baada ya safari ya awali kufutwa kutokana na nchi kadhaa kufuta ruhusa za kutumia anga zao.
Lai Ching-te alisema ziara yake ya awali “ilisitishwa kutokana na nguvu za nje zisizotarajiwa”.
“Natumaini safari hii itachangia kuimarisha zaidi urafiki kati ya Taiwan na Eswatini, kupitia uhusiano wa karibu zaidi katika uchumi, kilimo, utamaduni na elimu, pamoja na kuendeleza ushirikiano wa kimataifa wa Taiwan,” aliongeza.
















