Aliyekuwa kocha wa timu ya taifa ya soka ya Kenya ‘Harambee Stars’ Engin Firat amefariki dunia kwa mshtuko wa moyo akiwa katika uwanja wa ndege wa Istanbul, nchini Uturuki.
Firat, raia wa Uturuki ambaye aliifundisha ‘Harambee Stars’ kati yam waka 2021 na 2024, amefariki dunia Machi 9, 2026, wakati akirejea nyumbani kutoka jijini Beirut, Lebanon, ambako anafundisha klabu ya Nejmeh.
Taarifa ya Nejmeh ilithibiitisha kifo cha kocha huyo, huku ikimsifia kwa weledi wake katika kipindi chote alichoinoa timu hiyo.
“Sisi ni wa Mungu na kwake tutarejea. Kwa huzuni na masikitiko makubwa klabu yetu inamlilia kocha wetu wa kikosi cha kwanza, Engin Firat aliyetangulia mbele za haki kwa mshtuko wa moyo katika Uwanja wa Ndege wa Istanbul akiwa njiani kuelekea Adana, saa chache baada ya kuondoka Beirut kwenda nchini mwake.
“Katika kipindi alichofanya kazi na klabu, marehemu alitambulika kwa weledi wa kujitolea na maadili ya hali ya juu na ameacha muonekano mzuri kwa timu na wanafamilia wa Nejmeh,” ilisomeka sehemu ya taarifa ya klabu hiyo.














