Uturuki itaendelea kufuatilia juhudi za maendeleo na ustawi licha ya migogoro katika eneo hilo, amesema Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan.
“Uturuki iko kwenye njia sahihi, Mungu akipenda. Mwelekeo wake uko wazi, kwa hali yoyote itafika inakokwenda,” Erdogan amesema katika hotuba yake baada ya kikao cha Baraza la Mawaziri kilichoongozwa na yeye mjini Ahlat, Bitlis, Jumanne.
“Uturuki iko salama. Dhamana iliyokabidhiwa katika mikono salama, inayowakilisha watu milioni 86, iko salama. Kwa hali yoyote hatutaruhusu dhamana hii takatifu kuwekwa kwenye kivuli,” aliongeza.
Baraza la Mawaziri lilikutana chini ya uenyekiti wa Erdogan katika Ikulu ya Rais ya Ahlat.
Erdogan amesema kikao hicho kilijadili masuala mbalimbali, yakiwemo sera za nje, biashara, usalama na mchakato wa serikali wa “Uturuki Isiyo na Ugaidi.”
Alisema migogoro ya kiuchumi ya kikanda inaathiri Uturuki, lakini serikali itaendelea kushikilia malengo yake katika ajira, mauzo ya nje, kilimo na utalii.
Akizungumzia athari za kiuchumi za mvutano kati ya Iran na Marekani, Erdogan amesema: “Kadiri mshtuko uliosababishwa na mvutano kati ya Iran na Marekani katika uchumi wa dunia unavyozidi kupungua hatua kwa hatua kadiri muda unavyopita, tutapata fursa ya kuona kwa uwazi athari zake katika maisha ya kila siku.”
Mchakato wa “Uturuki Isiyo na Ugaidi”
Akizungumzia mchakato wa “Uturuki Isiyo na Ugaidi,” Erdogan amesisitiza umuhimu wa sheria iliyoidhinishwa hivi karibuni na Bunge kwa kura 467, akiitaja kuwa makubaliano ya kihistoria na kusema kuwa imeuimarisha mchakato huo.
“Demokrasia ya Uturuki ina ukomavu wa kutatua tatizo lolote inapofanya kazi kwa uelewa unaoweka nchi na taifa mbele, badala ya hesabu za kisiasa za kila siku,” alisema.
Erdogan aliwataka watu wenye mitazamo yote ya kisiasa kuchangia katika mchakato huo, akisema suala hilo linaihusu dola nzima na watu wake milioni 86, badala ya kuwa jukumu la serikali na muungano wake pekee.
“Njoono, tutimize ipasavyo deni letu la shukrani kwa mashahidi wetu na maveterani kwa kuiondoa Uturuki katika ugaidi,” Erdogan amesema.
Ameonya kwamba hatua yoyote inayofanya mchakato huo kuwa mgumu, kuuhujumu, kuuchochea au kuupinga itawajibishwa mbele ya historia.
Erdogan pia amezitaka taasisi za kiraia na wadau wengine katika eneo hilo kuongeza mchango wao katika mchakato huo.
Migogoro ya kikanda na amani
Akizungumzia migogoro ya kikanda, Erdogan amesisitiza tena juhudi za Uturuki za kukuza amani.
“Uturuki inapotafuta amani kwa kila mtu katika eneo lake, pamoja na wananchi wake, mipango ya mitandao ya kihalifu iliyojengwa juu ya damu na migogoro inavurugwa,” alisema.
“Tunaona mipango ya umwagaji damu inayotengenezwa kwa ajili ya eneo letu. Mungu akipenda, hatutaruhusu itekelezwe.”
Erdogan aliongeza kuwa Uturuki haitaacha kufanya kazi ya kuleta amani katika eneo hilo kwa sababu baadhi ya watu hawataki amani hiyo, wana wasiwasi nayo au wanaona mipango yao ikivurugwa.
Amesema Uturuki itaendelea kuunga mkono juhudi za majirani zake za kurejea katika hali ya kawaida na kujijenga upya, licha ya upinzani kutoka kwa kile alichokiita “mitandao ya kihalifu yenye damu ya watu wasio na hatia mikononi mwao.”
“Hatuna ajenda wala nia iliyofichika, kinyume na madai ya baadhi ya watu. Lengo letu ni kuona mazingira ya amani yakitawala katika maeneo yanayotuzunguka,” Erdogan amesema.






















