Wake wa viongozi wa Afrika: Janet Museveni wa Uganda

Janet Museveni amekuwa mwanasiasa na mke wa rais wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki tangu 1986 wakati mume wake Rais Yoweri Museveni alipochukua uongozi.

By Coletta Wanjohi
Janet Museveni ni mke wa Rais wa Uganda / Reuters

Mke wa Rais wa Uganda ni Janet Kataha Kainembabazi Museveni alizaliwa Juni 24, 1948.

Amekuwa mwanasiasa na mke wa rais wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki tangu 1986 wakati mume wake Rais Yoweri Museveni alipochukua uongozi.

Wamejaaliwa kupata watoto wanne. Mtoto wao Muhoozi Kaineruganba ndiye mkuu wa jeshi la Uganda.

Janet Museveni alienda uhamishoni mwaka 1971 hadi Tanzania wakati kiongozi wa wakati huo Idi Amin alipopindua utawala katika mapinduzi ya kijeshi.

Aliolewa na Yoweri Museveni Agosti 1973.

Wakati wa utawala wa Idi Amin ulipoanguka  Aprili 1979, alirejea Uganda.

Lakini Februari 1981 Janet na watoto wake walihamia tena Nairobi, Kenya, ambako waliishi na marafiki wa familia hadi 1983. Wakati huo Museveni na wanajeshi wengine wakiwa msitumi wakipigana kuiondoa serikali ya wakati huo madarakani.

Mwaka 1983, walienda Uswidi, na kukaa huko hadi Mei 1986, hii ilikuwa miezi minne baada ya Jeshi la Taifa la Yoweri Museveni kunyakua mamlaka huko Kampala.

Janet Museveni ana Shahada ya Kwanza ya Elimu kutoka Chuo Kikuu cha Makerere Uganda. Pia ana Stashahada ya Ukuzaji wa Utotoni kutoka Uswidi.

Aliingia katika siasa 2006 akianza kwa kuwa mbunge.

Baadae alichaguliwa tena Machi 2011 kwa muhula mwingine wa miaka mitano.

Akiwa bado mbunge, Februari 2009 Rais Museveni alimteua kuwa Waziri wa eneo la Masuala ya Karamoja na baadaye Waziri wa Elimu, wadhifa anaoshikilia hadi sasa.

Kando na siasa na kuwa mke wa Rais wa Uganda Janet Museveni, tangu 1986 alianzisha Juhudi za Wanawake wa Uganda Kuokoa Yatima (UWESO), shirika  ambalo linashughulikia mayatima wenye maambukizi ya virusi ya Ukimwi.

Pia ni mwanzilishi wa shirika ambayo linafanya kazi na wanawake maskini wa vijijini ili kuwawezesha kiuchumi.

Kimataifa, anatambuliwa kwa juhudi za kutetea uzazi salama. Na kuwa kiongozi katika hospitali maalum ya watoto walemavu nchini Uganda.

Mtindo wake wa nywele fupi za asili ulipata umaarufu nchini na sasa unaitwa "Janet cut" huku wanawake wengi wakiiga kwa sababu ya urahisi wake.