Utajiri wa Afrika: Timbila, sauti ya muziki ya Msumbiji
Timbila ni ala inayotengenezwa kwa ustadi mkubwa kutokana na mbao zilizosawazishwa zenye sauti mbalimbali.
Katika jamii ya Chopi nchini Msumbiji, mziki na uchezaji wake haukamiliki bila ala ya mziki iitwayo timbila.
Ni urithi ambao shirika la UNESCO linautambua tangu 2008 kama Turathi za Kitamaduni.
Jamii ya Chopi inaishi kusini mwa mkoa wa Inhambane ambao uko kusini mwa Msumbiji na ni maarufu kwa mziki wao wa okestra.
Timbila ni ala inayotengenezwa kwa ustadi mkubwa kutokana na mbao zilizosawazishwa zenye sauti mbalimbali.
Mbao hizo zinatokana na mti wa mwenje unaokua polepole.
Chini ya kila ubao, kitoa sauti kilichotengenezwa kwa vibuyu hufungwa vizuri kwa nta, na kukolezwa kwa mafuta kutoka kwa mti unaoitwa nkuso, hivyo kuipa timbila sauti ya kipekee yenye mitetemo.
Okestra zao zina tofautiana kwa ukubwa na sauti.
Wataalamu wa timbila huwa na wanafunzi wa rika zote, mara nyingi watoto wakicheza karibu na babu zao.
Kila mwaka, nyimbo mpya zinazotumia kutumia timbila hutungwa na kuchezwa kwenye shughuli mbalimbali za kijamii ikiwem harusi.
Ustadi wa kucheza ala hii ya mziki ni wa kipekee kwani mkono wa kushoto wa mchezaji mara nyingi unatekeleza mdundo tofauti na ule wa mkono wa kulia.
Tumbuizo hii hudumu kwa takriban saa moja.
Wasanii wengi wenye uzoefu wa timbila sasa ni wazee.
Ingawa wataalamu kadhaa wa kucheza timbila wameanza kutoa mafunzo kwa chipukizi, mafunzo hayo pia yanajumuisha wasichana katika vikundi vyao vya okestra na densi, UNESCO ina wasiwasi kuwa vijana wanazidi kupoteza mawasiliano na urithi huu wa kitamaduni kwa sababu wa mitindo ya kisasa ya maisha.