Umuhimu wa mashabiki mchezoni

Hivi ni kweli mchezo haunogi bila mashabiki? Kwani mashabiki wanachangia kwa kiasi gani kwa timu ya nyumbani kupata ushindi?

By Wazir Khamsin
Shabiki wa Jamhuri wa Kidemokrasia ya Congo (DRC). /Wengine


Katika michezo shabiki amepewa jina la mchezaji wa 12 na wataalamu wanasema wanasaidia katika saikolojia ya mchezo, na naam kwa asilimia kubwa wanaweza wakawa chachu ya ushindi kwa timu ya nyumbani.

Wanakuwa na mbwembwe aidha kwa mavazi au nyimbo za ushabiki ambazo mara nyingi zinakuwa zinahamasisha wachezaji.

Wanasema kuna sababu kwa nini ikaitwa mchezo wa nyumbani una faida kwa timu ya nyumbani. Katika kudadavua hili baadhi ya wataalamu wanasema mashabiki wana uwezo wa kuipa ushindi timu ya nyumbani kwa hadi asilimia 65.

Wanakwenda mbali zaidi na kusema magolikipa wanaozomewa na timu pinzani, wanaweza kupoteza penati kwa asilimia 15 kutokana na mchecheto kama hawako makini golini.

Pamoja na nguvu ya mashabiki na umahiri wao, siku zote inasemekana timu ya nyumbani inakuwa na shinikizo zaidi kuliko wageni na hili huenda likawafanya wateleze katika kumakinika kwao.

Mara nyingi mashabiki huwapa motisha wachezaji haswa wakati wanapojihisi wamechoka, nyimbo na hamasa huwapa matumaini.

Alafu kuna mashabiki ambao wanajulikana kama joka la mdimu yaani hayuko upande wowote ila anaitakia mabaya moja ya timu.

Ukweli ni kuwa mchezaji wa kumi na mbili ni muhimu iwe kwa timu wenyeji kwa maana ya nyumbani au kwa timu ya ugenini.

Lakini je, inawezekana ushawishi wa mashabiki kindakindaki ukafanikiwa kupindua meza?