Uganda: Wataalam wataka kituo maalum cha kutibu majeraha ya moto katika eneo la uzalishaji mafuta

Wataalamu wa matibabu nchini Uganda wameiomba serikali kuweka kituo maalumu cha matibabu ya moto katika eneo inalopanga kuweka kituo cha uzalishaji wa mafuta.

By
Uganda inapanga kuanza uzalishaji wa mafuta 2026. / Reuters

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kiruddu ya Uganda, Dkt. Charles Kabugo, ametoa wito wa kujengwa kwa hospitali nyingine maalum kwa ajili ya matibabu ya walioungua karibu na eneo la uzalishaji wa mafuta, akitaja uwepo wa ongezeko la ajali za moto kutokana na uzalishaji wa mafuta.

Hospitali ya Taifa ya Rufaa ya Kiruddu iko katika mji mkuu wa Kampala ambao uko zaidi ya kilomita 200 kutoka wilaya ya Hoima ambako uchimbaji wa mafuta unaendelea.

"Kama nchi tumeingia kwenye utafutaji wa mafuta na gesi, ukiingia kwenye utafutaji wa mafuta na gesi hatari ya moto inakuwa kubwa," alisema.

Alitoa wito huo alipofika mbele ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, wakati wa kujadili taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya mwaka 2024/25.
Alibainisha kuwa maeneo ambayo utafutaji wa mafuta hufanyika yanahusisha milipuko ya mara kwa mara.

Aliongeza kuwa iwapo maafa kama hayo yangetokea, Hospitali ya Kiruddu haitakuwa na uwezo wa kutosha wa kushughulikia ongezeko la wagonjwa walioungua kama inavyoonekana katika nchi nyingine zinazotafuta mafuta.

"Hiyo ina maana kwamba kwa hakika tunahitaji kitengo kikubwa zaidi ambacho kinapaswa kuwa na uwezo wa kusimamia aina hii ya wagonjwa. Tuko katika mchakato wa kuandaa pendekezo ambalo tunataka kuliwasilisha kwa serikali," Dk. Kabugo alisema.

Kulingana na Hospitali ya Kiruddu, pendekezo ambalo linajadiliwa linahusisha kuanzisha nafasi kubwa ambapo kitengo cha walioungua kinaweza kuhama ili kuweza kudhibiti majeraha makubwa na kushughulikia hali ambapo majanga kama hayo yanaweza kusababisha vifo vingi vya takriban wagonjwa 100.

"Kwa sasa, nadhani kama nchi hatujajiandaa kwa hilo. Tuna changamoto za nafasi katika hospitali zetu kwa sasa na hata kitengo cha matibabu ya majeraha ya moto ya kawaida hakitoshi kwa sasa,” Dk. Kabugo alisema.

Uganda inapanga kuanza uzalishaji wa mafuta mnamo 2026.