Kufikia mwisho wa mwaka 2025, Sudan bado iko kwenye vita vikubwa. Ingawa mji mkuu wa Khartoum uko tena chini ya udhibiti wa jeshi, nchi imegawanyika, makubaliano ya kusitisha mapigano yameshindikana, hivyo kuufanya mgogoro huo mbaya zaidi kushuhudiwa katika historia ya binadamu duniani.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu milioni 30 wanahitaji msaada wa haraka, wakati ambapo mamilioni wamekimbia makazi yao.
Tukio kubwa zaidi la mwaka 2025 lilitokea Machi, wakati Jeshi la Sudan (SAF) lilipofanikiwa kuurejesha mji wa Khartoum katika himaya yake baada ya karibu ya miaka miwili ya mapigano.
Jeshi lilichukua tena Ikulu ya Rais, majengo ya serikali, na uwanja wa ndege wa kimataifa, na kuwalazimisha wapiganaji wa RSF kuondoka katika sehemu kubwa ya mji mkuu. Huu ulikuwa ushindi mkubwa zaidi kwa jeshi tangu vita kuanza.
Hata hivyo, vita havijakwisha huku kila jitihada ya mazungumzo ya kuleta amani ikigonga mwamba.
Mauaji ya halaiki
Eneo la Darfur, lililoathirika tayari na migogoro ya awali, liligeuka tena kuwa kitovu cha mateso ya raia.
Mwaka 2025, RSF ilizidi kuimarisha udhibiti wake katika sehemu kubwa ya Darfur, huku mji wa El Fasher, mji mkuu wa Darfur Kaskazini ukizingirwa na RSF kwa zaidi ya siku 500. Raia walinaswa katikati ya mapigano, wakikosa chakula, maji, na huduma za afya. Kambi za wakimbizi zilishambuliwa, na familia zilizokwishakimbia hapo awali zililazimika kukimbia tena.
Aprili 2025, shambulio dhidi ya kambi ya Zamzam lililotekelezwa na RSF lilikuwa mojawapo ya matukio mabaya zaidi ya vita hivi. Ndani ya siku chache, mamia ya raia waliuawa na maelfu walifurushwa.
Ripoti za Umoja wa Mataifa zilithibitisha mauaji ya zaidi ya raia 1,000 katika shambulio hilo pekee, pamoja na ushahidi wa mashambulizi dhidi ya masoko, hospitali, na makazi ya raia.
Kwa wachunguzi wa haki za binadamu, kilichotokea El Fasher hakikuwa tukio la kawaida la vita—kilikuwa kielelezo kinachoweza kutajwa kama uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu, kikikumbusha dunia maafa ya Darfur ya miaka ya 2000.
Vita vilivyovuka mipaka ya Sudan
Vita vya Sudan havikubaki ndani ya mipaka yake. Kufikia mwisho wa 2025, mgogoro huu ulikuwa mkubwa zaidi wa uhamishaji wa watu duniani. Zaidi ya watu milioni 14 walikuwa wamelazimika kuyahama makazi yao, wengine wakikimbia ndani ya nchi, na wengine wakivuka mipaka kwa hofu ya maisha yao.
Mamilioni walikimbilia nchi jirani ambazo tayari zilikuwa dhaifu. Chad ililemewa na wimbi la wakimbizi kutoka Darfur. Misri ilipokea maelfu ya familia za Sudan, wengi wao wakikabiliwa na gharama kubwa za maisha. Sudan Kusini, yenyewe ikitoka katika migogoro ya muda mrefu, ililazimika kuwahudumia wakimbizi.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, uhamishaji huu mkubwa umeathiri mifumo ya afya ya eneo zima la Pembe ya Afrika. Magonjwa yameenea kwa kasi, kambi zimejaa kupita kiasi, na nchi jirani sasa zinabeba mzigo wa vita ambavyo havikuanza kwao.
Njaa na kuporomoka kwa huduma za maisha
Kadiri risasi zilivyoendelea kurindima, njaa ilienea kimya kimya. Kilimo kiliharibiwa, masoko yakafa, na njia za misaada zikakatwa. Mamilioni ya watu walijikuta wakikabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, huku mashirika ya misaada yakionya kuwa Sudan ilikuwa ikielekea katika mojawapo ya majanga makubwa zaidi ya njaa katika historia yake.
Mfumo wa afya ulisambaratika. Hospitali nyingi zilifungwa, chanjo zikatoweka, na magonjwa yanayoweza kuzuilika yakaenea kwa kasi katika kambi za wakimbizi. Wanawake wajawazito, watoto, na wazee walikuwa katika hatari kubwa zaidi.
Watoto wa Sudan wamekuwa wahanga wakuu wa vita hivi. Mamia ya maelfu wanaugua utapiamlo mkali, huku mamilioni wakikosa elimu kwa miaka kadhaa mfululizo. Hofu kubwa sasa ni kupotea kwa kizazi kizima kilichokulia katika kivuli cha vita.
Licha ya ukubwa wa janga hilo, juhudi za kimataifa za kusitisha vita hazikufua dafu. Makubaliano ya muda na mazungumzo yamekwama, na Sudan ikazidi kusahaulika katika ajenda ya dunia. Wakati huo huo, ushahidi wa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu uliendelea kujikusanya bila hatua madhubuti za kuwawajibisha wahusika.
Ukosefu wa haki umeendeleza mzunguko wa vurugu, huku raia wakiachwa bila ulinzi wala matumaini ya haki.
Vita vya Aprili 2023
Ili kuelewa chanzo cha hali hii, ni lazima turudi Aprili 2023.
Baada ya vuguvugu ya mwaka 2019 na kushindwa kwa serikali ya mpito wa utawala wa kiraia, mvutano ulizuka kati ya washirika wa zamani: jeshi la taifa la Sudan na kikosi cha wanamgambo cha RSF. Mapambano ya madaraka yaligeuka kuwa vita kamili.
Kadri mwaka 2025 unavyomalizika, Sudan bado imegawanyika, raia wake wakinaswa kwenye vita visivyo na mwisho unaoonekana.
Vita hivi vimesababisha vifo vya maelfu ya watu na kuwafanya mamilioni ya wengine kuyahama makazi yao.


















