Cameroon imesema kuwa raia wake 16 wameuawa wakipigana upande wa Urusi katika vita vya Ukraine
Wizara ya mambo ya nje ya Cameroon imezitaka familia za waliouawa kuwasiliana na maafisa wa wizara hiyo walioko katika mji mkuu, Yaoundé.
Cameroon ilisema mamlaka ya Urusi imethibitisha vifo vya raia wa Cameroon 16 wanaopigana dhidi ya Ukraine, ikiwa ni mara ya kwanza kwa nchi hiyo ya Afrika ya Kati kuzungumza kuhusu kuhusika kwa raia wake katika vita vinavyoendelea kati ya Urusi na Ukraine.
Katika taarifa iliyotangazwa kupitia vyombo vya habari vya serikali Jumatatu jioni, wizara hiyo ilizitaka familia za waliokuawa kuwasiliana na maafisa wa wizara katika mji mkuu wa Yaoundé.
Hati ya kidiplomasia ya Cameroon, pia ya siku ya Jumatatu iliyoonekana na Reuters, iliwataja waliouawa kuwa “wakandarasi wa kijeshi wenye uraia wa Cameroon” waliokuwa wakifanya kazi katika eneo la operesheni maalum ya kijeshi — neno linalotumiwa na Urusi kuelezea vita vya Ukraine.
Taarifa hiyo na hati ya kidiplomasia hazikueleza jinsi watu hao 16 walivyofika kupigana upande wa Urusi, wala kutoa maelezo kuhusu mahali, muda, au mazingira ya vifo vyao.
Ubalozi wa Urusi mjini Yaoundé haukutoa ufafanuzi kwa shirika la habari la Reuters.
Kuajiri raia wa Afrika
Ukraine ilisema mwezi Februari kuwa zaidi ya raia wa Afrika 1,700 wanapigana upande wa Urusi. Mamlaka ya Urusi imekanusha kuwahamasisha au kuwaajiri kinyume cha sheria raia wa Afrika kupigana nchini Ukraine.
Katika nyaraka ya ndani iliyotolewa Machi 2025 na kuonekana na Reuters, waziri wa ulinzi wa Cameroon alionyesha wasiwasi kwamba wanajeshi walikuwa wanaondoka nchini humo ili kujiunga na vita vya Ukraine, na aliwaagiza makamanda kufuatilia kwa karibu vikosi vyao.
Cameroon imesema kuwa haitumi wanajeshi wake nje ya nchi isipokuwa chini ya mamlaka ya kimataifa au kikanda, na imeonya raia wake dhidi ya kushiriki katika migogoro ya kigeni.