Madagascar yatibua njama ya kumuua rais: mwendesha mashtaka

Kanali wa jeshi na washukiwa wengine 12 wanakabiliwa na mashtaka ya kupanga kumuua Rais Michael Randrianirina.

By
Rais Michael Randrianirina aliingia madarakani Oktoba 2025 kufuatia maandamano ya kuipinga serikali ya Andry Rajoelina. / / AP

Watu kumi na watatu, akiwemo kanali wa jeshi, wanakabiliwa na mashtaka nchini Madagascar kufuatia njama iliyotibuliwa ya kumuua Rais Michael Randrianirina.

Mwendesha mashtaka wa umma nchini Madagascar, Narindra Rakotoniaina, alisema kuwa watu 11 kati ya hao 13 wako rumande.

Hata hivyo Kanali Patrick Rakatomamonjy, mmoja wa waandaaji wakuu, bado hajakamatwa.

Rakotoniaina alitaja ujumbe wa maandishi na wa WhatsApp kati ya kundi hilo kama ushahidi wa njama hiyo, akiongeza kuwa nyumba za baadhi ya wanachama zilifanyiwa upekuzi.

“Baadhi ya waliokamatwa wamekiri kuwa ariary bilioni 20 (dola milioni 4.8) zilizopatikana kwenye akaunti za benki zilikuwa zitatumika kutekeleza mipango yao,” Rakotoniaina alinukuliwa akisema na gazeti la ndani L'Express De Madagascar siku ya Ijumaa.

Randrianirina, ambaye ni kanali wa jeshi, alichukua madaraka Oktoba iliyopita baada ya wimbi la maandamano yaliyoongozwa na vijana kuhusu ukosefu wa umeme na maji kumng’oa madarakani rais wa wakati huo Andry Rajoelina, ambaye alitoroka nchini humo.

Katika ziara yake mjini Malabo, nchini Equatorial Guinea wiki moja iliyopita, Randrianirina aliwaambia wanachama wa diaspora ya Malagasy kwamba yeye na mke wake walikuwa walengwa wa jaribio la kuuawa, na kwamba watu walikuwa tayari wamekamatwa.