Kenya inaimarisha usalama kuelekea mwishoni mwa juma wakati mashindano ya Safari Rally yakitarajiwa kuvutia maelfu ya mashabiki katika Kaunti ya Naivasha ambako michuano hiyo inafanyika.
Mashindano hayo ya kila mwaka yanaanza tarehe 12 hadi 15 Machi yakishirikisha madereva 46, wakiwemo 17 kutoka Kenya, 4 kutoka Uganda na 4 kutoka Rwanda.
"Zaidi ya maafisa wa polisi 1000 kutoka vikundi mbalimbali watapelekwa katika njia za makutano, maeneo ya watazamaji na barabara kuu za kufikia ili kuhakikisha hali ya usalama, pamoja na kudhibiti umati wa watakaojitokeza na kusaidia udhibiti wa msongamano wa magari," Wizara ya Mambo ya Ndani ilisema katika taarifa yake.
Madereva watashindana kupitia hatua 20 maalum kwa siku nne zinazojumuisha jumla ya kilomita 338.
Wizara ya Mambo ya Ndani na Utawala wa Kitaifa imepiga marufuku utumiaji wa ndege zisizo na rubani katika maeneo yaliyotengwa ndani ya Naivasha na maeneo jirani wakati wa WRC Safari Rally Kenya 2026. Imesema hii ni ehemu ya hatua za usalama kwa watazamaji wa mashindano hayo yanayoingia siku ya pili.
Mashindano ya mwaka huu yatakuwa na changamoto kidogo kwa sababu barabara zimejaa maji na matoke, kutokana na msimu wa mvua unaoendelea.
Fursa ya utalii nchini Kenya
Tofauti na miaka mengine, mashindano ya WRC Safari Rally Kenya 2026 mwaka huu yalikosa uzinduzi rasmi unaofanywa na mkuu wa nchi jijini Nairobi.
"Tangu 1953, eneo letu limekuwa jaribio kwa madereva. Kuanzia mchanga wa Kedong hadi kwenye miamba ya Sleeping Warrior, tunatoa changamoto ambayo hakuna nchi nyingine inayoweza kuiga,” Rebecca Miano, Waziri wa Utalii wa Kenya alisema.
“Zaidi ya vumbi hili, Safari Rally ni injini ya mabilioni ya shilingi. Inaendesha asilimia 100 ya hoteli za mitaani, umiliki wa hoteli za Nakuru kwa asilimia 100. Pia ni asili ya ajabu kwa zaidi ya watazamaji milioni 80 ulimwenguni," Miano aliongezea.
Wikiendi ya Safari Rally mara nyingi huwavutia watu kutoka duniani kote.
Mashabiki kutoka nchi jirani za Uganda na Tanzania kwa mfano tayari wamepiga kambi Naivasha wakifurahia tamasha litakalotifua vumbi na matope.
"Zaidi ya msisimko ambapo vumbi huinuka na injini kuunguruma - magari yanapita katika mandhari ya kuvutia ya Kenya, kutoka maeneo ya ajabu ya Bonde la Ufa hadi nyanda za Hifadhi ya Kitaifa ya Hell's Gate, na maji tulivu ya Ziwa Naivasha," Bodi ya Utalii ya Kenya ilisema katika akaunti yake ya X.
Kulingana na Safari Rally Kenya, mashindano ya WRC Safari Rally ya 2025 yalivutia zaidi ya watu 400,000, idadi kubwa zaidi ya waliohudhuria tangu tukio hilo kurejea Kenya mwaka wa 2021.














