Tanzania miongoni mwa nchi zilizopigwa marufuku kusafiri Marekani
Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zilizoathiriwa na hatua mpya za serikali ya Marekani za kudhibiti uingiaji wa raia wa baadhi ya mataifa nchini humo.
Hatua hizi zilitangazwa na serikali ya Rais wa Marekani Donald Trump, na zinaweka vikwazo vya usafiri na viza kwa raia wa nchi husika.
Trump pia aliweka vizuizi vya muda vya kusafiri Marekani kwa raia wa nchi zingine za Kiafrika zikiwemo Nigeria, Ivory Coast, Senegal, Angola, Gabon, Gambia, Malawi, Mauritania, Zambia na Zimbabwe.
Kwa Tanzania, hatua hii sio marufuku kamili ya kusafiri kwenda Marekani.
Badala yake, Marekani imeamua kupunguza na kudhibiti baadhi ya aina za viza zinazotolewa kwa Watanzania.
Hii ina maana kwamba bado kuna Watanzania wanaoweza kusafiri kwenda Marekani, lakini njia fulani za kupata viza zimekuwa ngumu zaidi.
Serikali ya Marekani inaeleza kuwa uamuzi huu umetokana na changamoto za kiutawala, ikiwemo upungufu wa taarifa za uhakiki kwa waombaji wa viza, masuala ya usalama wa hati za kusafiria, pamoja na hali ya baadhi ya wasafiri kubaki Marekani baada ya muda wa viza zao kuisha.
Kwa vitendo, hatua hizi zinawaathiri zaidi Watanzania wanaoomba viza mpya, hasa wale wanaotafuta makazi ya kudumu (green card) au kushiriki bahati nasibu ya viza ya Marekani (DV Lottery).
Baadhi ya viza za muda, kama za kazi au ziara, zinaweza kuchelewa au kufanyiwa uchunguzi wa kina zaidi.
Hata hivyo, Watanzania ambao tayari wana viza halali, wanadiplomasia na wakaazi halali wa Marekani kwa ujumla bado wanaruhusiwa kuingia nchini humo.
Mpaka sasa serikali ya Tanzania haijasema lolote kuhusu hatua hiyo.