Waziri Mkuu wa Tanzania, Mwigulu Nchemba amesema kuwa serikali ya nchi inatambua uwepo wa watumishi wa umma wanaochapakazi na kuwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii na uadilifu huku wakijiepusha kujiingiza katika makundi ya wazembe, wezi na wanaofanya kazi kwa mazoea.
“Serikali haitomuonea mtu, watumishi wachapakazi wasiingie ubaridi kwa sababu serikali inatambua mchango wao katika maendeleo ya taifa,” alisema Nchemba siku Jumatatu.
Hali kadhalika, Waziri Mkuu huyo wa Tanzania ametumia fursa hiyo kuwasisitiza watumishi wa umma kufanya kazi kwa weledi na kujiepusha na vitendo vya udokozi kwa sababu havikubaliki na havivumiliki, hivyo wahakikishe wanatekeleza majukumu yao ikiwemo kusimamia ipasavyo ujenzi wa miradi.
Pia, alisisitiza mikoa yote nchini Tanzania kuhakikisha katika upangaji wa bajeti wanaweka vipaumbele vya uchimbaji wa visima kupitia mitambo iliyosambazwa katika mikoa yao.
“Mitambo ya uchimbaji maji itumike kuchimba visima ili wananchi wapate maji ya uhakika,” alieleza.
Wakati huo huo, Nchemba amezitaka mamlaka husika kuangalia uwezekano wa kuweka utaratibu au sheria itakayowabana wakandarasi kuhakikisha wanawalipa wafanyakazi wao stahiki zao kwa wakati.
Ametoa agizo hilo kutokana na kumekuwapo kwa malalamiko ya baadhi ya wakandarasi kutowalipa wafanyakazi wanaofanya kazi katika miradi ya ujenzi hata pale wanapokuwa wameshalipwa na Serikali kwa kazi walizotekeleza.

















