Ramadhan mjini Mombasa: Utamaduni, fursa na mabadiliko ya kijamii
AFRIKA
4 dk kusoma
Ramadhan mjini Mombasa: Utamaduni, fursa na mabadiliko ya kijamiiKatika mji wa pwani wa Mombasa, kuwasili kwa mwezi mtukufu wa Ramadhan huleta zaidi ya mabadiliko ya kalenda—huashiria mageuzi makubwa ya maisha ya kila siku.
Waislamu wakiswali katika mji wa Mombasa. / Wengine

Mji wa Mombasa hubadilika kwa namna ya kipekee: kutoka pilikapilika za mchana hadi kuwa na utulivu, kisha hali inakuwa tofauti tena jioni kwa shamrashamra na jamii kuchangamka.

 Ramadhan, mwezi wa tisa katika kalenda ya Kiislamu, ni kipindi ambacho Waislamu hujizuia na kula na kunywa kuanzia alfajiri hadi jioni, wakijikita katika ibada, mazingatio na matendo ya huruma.

Mji kubadilika na mifumo ya Imani

Katika kipindi hiki, ratiba za maisha hubadilika. Baadhi ya biashara hufungwa mapema ili kutoa nafasi kwa ibada. Misikiti hujaa waumini, hasa wakati wa swala za usiku kama taraweh na tahajjud. Sauti za adhana husikika kila sehemu, zikiashiria nyakati za swala na kufuturu. Hata hivyo, uzuri halisi wa Ramadhan ya Mombasa hujitokeza zaidi wakati wa jioni.

 Upatikanaji wa futari: Ladha mahsusi ya mji

 Kuanzia jioni hadi usiku, mitaa hubadilika kwa vyakula vya futari vinavyovutia. Meza hupangwa kandokando ya barabara zikiwa na vitafunwa vya asili ya pwani kama kaimati, viazi karai, sambusa, bajia, katlesi na tende. Harufu ya viungo vya Kiswahili huwa kila mahali, ikiwavuta wenyeji na wageni. Kwa bei nafuu, watu hupata fursa ya kuchagua vitafunwa wanavyovipenda— jambo linalogusa hisia zote. Kama anavyosema mwandishi wa habari, Yassin Juma:
 "Nimezunguka maeneo mengi, lakini Ramadhan ya Mombasa ina ladha ya kipekee. Hapa utamaduni huu bado unaishi kwa nguvu kuliko sehemu nyingi za Kenya."

 Fursa kwa vijana: uchumi wa msimu

 Ramadhan pia ni kipindi cha fursa za kiuchumi, hasa kwa vijana. Wengi hujishughulisha na biashara ndogo ndogo kama kuuza vitafunwa na vinywaji baridi, ikiwemo ‘‘slush’’. Maeneo kama mtaa wa Makadara huwa na shughuli nyingi jioni. Vijana hubuni njia za kujipatia kipato huku wakihudumia mahitaji ya waumini. Mfanyabiashara Fuad Mohd Ali anasema:"Hapa tunauza vitu vya kufuturu kama tende, viazi na bhajia. Hata mtu akiwa safarini anaweza kusimama na kufuturu kwa wakati. Hii imekuwa desturi yangu tangu nikiwa mdogo."

 Biashara za Usiku na mji kuchangamka

Kadri Ramadhan inavyoendelea, hasa katika kumi la pili na lile la mwisho, Mombasa hubadilika zaidi. Maduka ya nguo na biashara nyingine hufunguliwa hadi usiku wa manane, yakihudumia watu wanaotoka katika ibada au matembezi. Mji hung’aa kwa taa, na usiku huwa kumechangamka kuliko mchana. Mkazi wa mji wa Mombasa Ali Mahfudh anaeleza:
 "Huu ni mwezi wa baraka. Watu wasiojiweza hupata chakula, na misaada hutolewa kwa wingi. Usiku unakuwa kama mchana kwa ibada na shughuli."

Changamoto za Usalama

Pamoja na uchangamfu huu, changamoto za usalama zimejitokeza katika baadhi ya maeneo. Wenyeji wanatoa wito kwa serikali kuimarisha ulinzi, hasa wakati wa usiku ambapo watu wengi huwa nje. Mkazi wa Mombasa Salim Karama Jiwe anasema: "Tunathamini utulivu uliopo, lakini tungependa usalama uimarishwe zaidi ili watu waendelee na ibada zao bila hofu."

 Baadhi ya wakazi pia wamemuomba Rais William Ruto kuzingatia kupunguza gharama za maisha, hasa bei za vyakula muhimu wakati wa Ramadhan.

Utamaduni unaobadilika

Baadhi ya utamaduni wa zamani umeanza kuondoka. Majirani walikuwa wakipelekeana vyakula vya futari lakini sasa hali ni tofauti, ingawa bado ipo kwa baadhi ya familia.

 Vilevile, utamaduni wa watoto kupiga matwari au madufu na kuimba qaswida mitaani umepungua sana, ukibaki kama kumbukumbu katika maeneo machache.

 Zaidi ya Biashara: Hali ya mhikamano

Licha ya mabadiliko haya, kiini cha Ramadhan bado ni mshikamano wa kijamii. Ni wakati ambapo watu hukutana, kushirikiana na kusaidiana bila kujali tofauti zao. Majumbani, vyakula vya asili kama viazi vya nazi, ndizi zinazoungwa kwa nazi, samaki wa kupaka na mathobosha au vipopoo huandaliwa kwa wingi. Familia hukusanyika pamoja kufungua saumu—jambo linaloleta furaha, shukrani na upendo.

Sehemu ya maisha ya watu

 Ramadhan mjini Mombasa si mwezi wa ibada pekee—ni sehemu ya maisha ya watu na simulizi inayoendelea kuandikwa kila mwaka, ukibeba taswira ya kijamii, kiuchumi na kitamaduni.

 Ni harufu ya chai ya karafuu kila unapopita mitaani.
 Ni mchanganyiko wa sauti za swala na pilikapilika za sokoni jioni.
 Ni vijana wanaotafuta riziki, na jamii inayojitahidi kuhifadhi utamaduni wake.

 Kwa ufupi, Ramadhan ya Mombasa si jambo la muda mfupi tu—ni urithi unaoendelea kuishi, ukibadilika kizazi hadi kizazi huku ukidumisha kiini chake cha imani na utamaduni.

CHANZO:TRT Afrika Swahili
Soma zaidi
Rais Mohamud anasema Somalia haipingi wazo la Ethiopia kupata njia ya bahari
Kiongozi wa Somalia aapa kuzuia uwepo wa jeshi la Israel mjini Berbera
Viongozi wa Eritrea, Somalia, Sudan na Misri kufanya mazungumzo huku mivutano ikiongezeka Ethiopia
Rais wa Misri ataka suluhu za amani kwa migogoro kote barani Afrika
Vikosi vya serikali ya Ethiopia vyakomboa uwanja wa ndege katika mji mkuu wa Tigray
RSF 'iliwaua' zaidi ya raia 25 Kaskazini mwa Kordofan, katika ukiukaji wa sheria za kibinadamu
UN yapongeza maendeleo ya haki za binadamu nchini Somalia
Botswana yakosolewa kwa kuidhinisha kuuawa kwa tembo 23 kusherehekea Siku ya Uhuru
Meli yenye hospitali kubwa ya kiraia duniani yafika Ghana kwa mara ya tatu
Algeria yapitisha muswada wa adhabu ya kifo kwa wanaoanzisha moto wa nyika makusudi
AU yataka Ethiopia, Eritrea, Misri kusitisha uhasama unaosababisha ukosefu wa usalama katika kanda
Polisi nchini Zimbabwe wasema waliofariki katika ajali ya helikopta na Chivayo ni watano
Eritrea yakata mahusiano yote ya kidiplomasia na Ethiopia
Nigeria: Wanawake 3 wafariki katika msongamano wakati wa kugawiwa Fedha
Tunisia kutoza faini wanaosambaza 'taarifa za kupotosha’ badala ya kifungo kwa uhalifu wa mitandaoni
Mfanyabiashara Wicknell Chivayo afariki katika ajali ya helikopta Zimbabwe
Dangote kujenga kiwanda cha kusafisha mafuta Kenya kwa gharama ya $16 bilioni
Mfalme wa Morocco amteua El Mansouri waziri mkuu wa kwanza mwanamke
Rais wa Afrika Kusini aagiza hatua za kuwalinda wanawake kufuatia mfululizo wa mauaji
Misri yakana kuingilia mambo ya ndani ya Ethiopia na kuunga mkono makundi yenye silaha