Mvutano wa kidiplomasia unaendelea kuchacha kati ya Uganda na Marekani, na chanzo chake kilianzia mitandaoni.
Kiini cha mgogoro huo ni Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ambaye alichapisha ujumbe kwenye mitandao ya kijamii akidai kuwa Ubalozi wa Marekani mjini Kampala umeingilia masuala ya ndani ya kisiasa ya Uganda.
Mkuu huyo wa jeshi, ambaye pia ni mwana wa Rais Yoweri Museveni, alipendekeza kusitishwa kwa ushirikiano wa kijeshi kati ya Kampala na Washington, ikiwemo operesheni zao za pamoja za kiusalama katika eneo la Pembe ya Afrika.
Machapisho hayo pia yalimhusu mwanasiasa wa upinzani Bobi Wine na mara moja yakazua mjadala na mabishano makali. Ndani ya saa chache, ujumbe huo ulifutwa.
“Taarifa zisizo sahihi”
Baadaye, Jenerali Muhoozi alisema kuwa taarifa alizotegemea hazikuwa sahihi, na akathibitisha kuwa ushirikiano wa kijeshi kati ya Uganda na Marekani “utaendelea kama kawaida”.
Hata hivyo, huko Washington, maelezo hayo hayakutosha kutuliza wasiwasi. Mwenyekiti wa Kamati ya Mahusiano ya Kigeni ya Seneti ya Marekani, Seneta Jim Risch, alisema kuwa Jenerali Kainerugaba “amevuka mstari mwekundu”.
Seneta huyo alisema kuwa utawala wa Trump “lazima utathmini upya” ushirikiano wa kiusalama kati ya Marekani na Uganda, na ikiwezekana iwekewe vikwazo. Kwa mujibu wake, kufutwa kwa machapisho ya awali na kile alichokiita “msamaha usiyo na maana” kutoka kwa mkuu wa jeshi la Uganda haukutosha.
Hata hivyo, uongozi wa kijeshi wa Uganda umejibu vikali. Msemaji wa Wizara ya Ulinzi, Kanali Chris Magezi, alizitaja kauli za seneta wa Marekani kuwa ni “mbinu ya zamani ya kikoloni” ya vitisho na kuingilia “masuala ya ndani” ya Uganda, akisisitiza kuwa Uganda itapinga kwa nguvu mtazamo huo.
Trump bado hajatoa kauli yoyote
Kanali Magezi pia alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Uganda na Marekani ni wa kina katika sekta mbalimbali, na haupaswi kuathiriwa na mabishano ya hadharani kwenye mitandao ya kijamii.
Hadi sasa, Rais wa Marekani Donald Trump bado hajatoa kauli yoyote kuhusu mgogoro huo.
Muda huu unakuja baada ya uchaguzi wa hivi karibuni nchini Uganda, ambapo Rais Yoweri Museveni alishinfi muhula wa saba wa miaka mitano, na hivyo kuongeza utawala wake wa takribani miaka 40.
Hata hivyo, mpinzani wake mkuu Bobi Wine amekataa matokeo ya uchaguzi huo, akidai kulikuwa na dosari na udanganyifu, madai ambayo serikali imeyakanusha.














