| Swahili
UTURUKI
2 dk kusoma
Hali ya Mlango Bahari wa Hormuz irudi kama kawaida, asema Fidan
Kulingana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, mashambulizi ya kujibizana yanazidi kuzorotesha jitahada za amani ya kanda.
Hali ya Mlango Bahari wa Hormuz irudi kama kawaida, asema Fidan
Kulingana na Fidan, mashambulizi ya kujibizana, yanaendelea kuzorotesha jitihada za amani, akitoa wito kwa juhudi za haraka za kumaliza migogoro hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan ametoa wito wa kurejeshwa kwa hali ya kawaida ya Mlango Bahari wa Hormuz.

Akizungumza katika mkutano na wanahabari, akiwa na mwenzake wa Azerbaijan, Jeyhun Bayramov jijini Baku siku ya Jumanne, Fidan alibainisha kuwa, Uturuki na Azerbaijan, zina wasiwasi na kinachoendelea Iran.

 “Utulivu na ustawi wa Iran unaathari za moja kwa moja kwa kanda yetu. Hivyo basi, tungependa kuona mgogoro unaoendelea unamalizwa kwa njia za kidiplomasia, haraka iwezekanavyo,” alisema.

Kulingana na Fidan, mashambulizi ya kujibizana, yanaendelea kuzorotesha jitihada za amani, akitoa wito kwa juhudi za haraka za kumaliza migogoro hiyo.

“Wakati huo huo, ni vyema kwa shughuli mbalimbali katika Mlango Bahari wa Hormuz zikaendelea kama kawaida,” alieleza Fidan.

Akiangazia vita kati ya Urusi na Ukraine, Fidan amesema kuwa Uturuki inaendelea kujitahidi kuliepusha eneo zima la Bahari Nyeusi kuingia vitani.

Kulingana na Fidan, hilo lilifanikiwa kupitia mkataba wa Montreux na mradi wa nafaka wa Bahari Nyeusi.

“Hata hivyo, ongezeko la mashambulizi dhidi ya meli za kiraia katika bahari hiyo, linazidi kuhatarisha uhai, mali za watu na huduma za usafiri,” alisema Fidan.

Fidan alisema kuwa, Uturuki imeendelea kutoa maonyo kadhaa kwa pande zinazohitalifiana, ziweze kupata suluhu ya pamoja.

“Tutaendelea kufanya kila jitihada ili amani ipatikane,”alisema, akirejelea msimamo wa Rais Recep Tayyip Erdogan.

Hatari ya ongezeko la vita

Akijibu maswali ya wanahabari, Fidan alitadhaharisha kuwa, mgogoro kati ya Urusi na Ukraine umezidi kuendelea, ukiendelea kuhatarisha usalama wa maeneo mengine.

Ushirikiano kati ya Uturuki na Azerbaijan

Wakati huo huo, Fidan aligusia uhusiano wa kimkakati kati ya Uturuki na Azerbaijan.

Kulingana na Fidan, ushirikiano katika nyanja za kiuchumi, nishati na uchukuzi, unaendelea kuwa nguzo muhimu kati ya nchi hizo mbili.

Hali kadhalika, aliulezeka mradi wa reli ya Baku-Tbilisi-Kars, kama moja ya maeneo muhimu kwa nchi hizo mbili.

Pia, aligusia mpango wa kuimarisha muunganiko wa Uturuki na Azerbaijan kupitia Nakhchivan, ikiwemo njia ya Zangezur na mtandao wa reli ya Kars-Igdir-Aralik-Dilucu.

“Mungu akipenda, mradi wa reli ya Kars-Dilucu utakamilika kuelekea mwishoni mwa 2029,” alisema.

Kwa upande mwingine, Fidan aliweka wazi, kuwa Uturuki na Azerbaijan, zitaendelea kushirikiana kupitia mazoezi ya pamoja ya kijeshi na masuala mengine ya kiulinzi.

 

CHANZO:Anadolu Agency