Viwanja vya AFCON 2025 Morocco

Baada ya AFCON ya Morocco wanaopokea kijiti ni Afrika Mashariki ambao ndio watakuwa wenyeji wa AFCON 2027. Nchi hizo ni Kenya, Tanzania na Uganda.

By Wazir Khamsin
Uwanja wa Prince Moulay Abdellah mjini Rabat. /cafonline

Morocco ambao pia ni wenyeji wenza wa Kombe la Dunia 2030 wametumia mashindano ya AFCON kama sehemu ya maandalizi mazuri kuelekea huko.

Nchi hii inatumia viwanja 9 kwenye michezo ya mwaka huu, baadhi yao ikiwa vimekarabatiwa na kuongezwa idadi ya mashabiki katika miji mbalimbali.

Utakuwa unaukumbuka uwanja wa Prince Moulay Abdellah. Sherehe za ufunguzi zilifanyika hapa na ndipo ambapo fainali za mwaka zitakapochezwa. Uwanja huu ulioko katika mji mkuu wa Rabat una nafasi ya kuingia mashabiki 68,700.

Mechi zote za wenyeji Morocco zinachezwa hapo. Pia mechi moja ya robo fainali na nyingine ya nusu fainali pia zitapigwa katika uwanja huo.

Prince Moulay El Hassan uwanja huu pia uko mjini Rabat na una nafasi ya kuingia mashabiki 22,000. Mechi ya mwisho ya michuano hii itakuwa ya hatua ya 16 tarehe 6 Januari.

Uwanja mwingine mjini Rabat ni ule wa El Barid ambao pia unajulikana kama Al Madina. Uwanja huu ulioko katika wilaya ya Agdal ya mji mkuu unaweza ukawa na mashabiki 18,000 kwa wakati mmoja. Klabu ya Union Touarga hutumia kama uwanja wao wa nyumbani.

Pia kuna uwanja wa Olimpiki wa Rabat kilomita saba kutoka katikati ya mji, ambao una uwezo wa kubeba mashabiki 21,000.

Kisha kuna uwanja wa Tangier, mji ulioko kaskazini magharibi mwa Morocco. Uwanja huo wenye uwezo wa kuingia mashabiki 68,000 utakuwa na mechi moja ya robo fainali na nusu fainali moja ya tarehe 14 Januari.

Uwanja wa mji wa Marrakech ambapo kutachezwa robo fainali moja unaweza kuingia mashabiki 45,000.

Jijini Casablanca kuna uwanja wa Mohammed V ambao unapatikana kwenye wilaya ya Maarif wa mji huo. Mechi ya mshindi wa tatu Januari 17 itachezwa hapo na una uwezo wa kuingia mashabiki 67,000.

Katika mji wa kaskazini wa Fes au Fez ambao ni wa kihistoria una uwezo wa watu 45,000 sawa na ule mjini Agadir ambao uko kilomita karibu 500 kutoka mjini Rabat na hapo kutachezwa robo fainali moja ya tarehe 10 Januari.

Ukarabati na ujenzi wa viwanja kwa wenyeji wajao Afrika Mashariki unaendelea kwa sasa ili kuwa tayari kwa 2027, Je, kuna chochote cha kujifunza kutoka kwa maandalizi ya Morocco?