Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, akisisitiza kuwa hali ya taharuki katika kanda kwa mara nyingine imeonesha uhitaji muhimu wa kimkakati wa uhusiano wa Uturuki na EU.
Mazungumzo haya ya siku ya Jumanne yaliangazia uhusiano wa Uturuki na Muungano wa Ulaya pamoja na yanayojiri katika kanda na ulimwenguni, Kurugenzi ya Mawasiliano ya Uturuki ilisema kupitia mtandao wa kijamii wa Uturuki NSosyal.
Wakati wa mazungumzo hayo kwa njia ya simu, Erdogan alisema Uturuki imekuwa ikijitahidi kuhakikisha kuwa mapigano yanaendelea kusitishwa na kuwepo kwa amani katika mzozo unaoendelea kwenye kanda, akiongeza kuwa Mlango Bahari wa Hormuz pia unatakiwa kufunguliwa haraka iwezekanavyo.
Aliongeza kuwa Israel inataka kuendeleza mapigano katika kanda na inaendelea kukiuka sheria ya kimataifa, ikiwemo matukio yanayoelezwa kuwa uharamia, akisisitiza umuhimu wa jamii ya kimataifa kuzidisha shinikizo kwa Israel.
Rais wa Uturuki pia alisisitiza kujumuishwa kwa Uturuki katika mpango wa kimkakati wa usalama barani Ulaya kuwa itakuwa ni faida, kuwa Muungano wa Forodha wa Uturuki na EU unatakiwa kuimarishwa, na kwamba ushirikiano uendelezwe katika sekta zote ili kuimarisha ujumuishaji wa kiuchumi na maslahi ya pamoja.





















