Hispania imewarudisha nchini Morocco wahamiaji kadhaa kutoka Kusini mwa Jangwa la Sahara na bara Asia ambao walikuwa wamefika Ceuta na maombi yao ya hifadhi kukataliwa, ikiwa ni mara ya kwanza kwa wahamiaji kurudishwa tangu watu wengi walipovuka mpaka mwezi Julai.
Wizara ya Mambo ya Ndani inasema watu hao walirudishwa Morocco baada ya taifa hilo kukubali kuwachukua na kwa sasa wako nchini humo. Hispania ilikataa kueleza idadi au mataifa ya uraia wa wahamiaji hao lakini mashirika ya haki za binadamu na wahamiaji yaliyoko eneo la Ceuta yanasema watu 16 kutoka Senegal, Nigeria, Yemen, Cameroon, na Bangladesh walirudishwa.
Maelfu ya wahamiaji wamepewa makazi
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Hispania aliiambia Reuters kuwa Morocco inaaminika na Umoja wa Ulaya kuwa moja ya nchi salama, na kurudishwa kwa wahamiaji kunazingatia "taratibu zote za usalama", bila kutoa maelezo zaidi.
Kwa zaidi ya saa 48 mwezi Julai, watu karibu 80,000 walivuka kutoka Morocco hadi Ceuta, eneo la Hispania barani Afrika.
Pamoja na wahamiaji kadhaa kurudi baada ya siku chache, maelfu wengine walibaki na serikali ya Waziri Mkuu Pedro Sanchez inashinikizwa na wananchi kutatua tatizo la Ceuta kabla ya uchaguzi wa tarehe 29 Novemba.






















