| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Tanzania yatumia Dola milioni 9 kuagiza maziwa kutoka nje
Tanzania ni nchi ya pili kwa idadi kubwa ya ng'ombe barani Afrika, ikionyesha umuhimu wa sekta ya mifugo kiuchumi.
Tanzania yatumia Dola milioni 9 kuagiza maziwa kutoka nje
Kufikia mwaka 2025/2026, Tanzania ilikuwa na idadi ya ng'ombe inayokadiriwa kufikia milioni 39.24, ikiwa ni ongezeko la asilimia 3.4./Picha:Wengine
24 Machi 2026

Tanzania hutumia Dola milioni 8.9 kila mwaka (sawa na shilingi bilioni 23 za Kitanzania) kuagiza wastani wa lita milioni 11.6 za maziwa.

Hali hiyo inadaiwa kuchangiwa na changamoto za ubora wa miundombinu na elimu, miongoni mwa wadau wa sekta maziwa.

Akizungumza Machi 23, 2026, wakati wa mafunzo ya wakaguzi wa tasnia ya maziwa mjini Morogoro, Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), George Msalya,  amesema licha ya Tanzania kuzalisha takribani lita bilioni 4.1 za maziwa kwa mwaka, bado kuna pengo la uzalishaji linalosababisha nchi kuendelea kuagiza maziwa kutoka nje ili kukidhi mahitaji ya ndani.

Kulingana na Msalya, changamoto kubwa ni ubora wa maziwa yanayozalishwa na wadau wengi, hasa wa vijijini, kwani hawazingatii viwango vinavyotakiwa, hali inayowafanya walaji wengi kuamini kuwa maziwa ya nje ni bora zaidi kuliko yanayozalishwa nchini humo.

Kwa mujibu wa takwimu, Tanzania ina jumla ya viwanda 188 vya kusindika maziwa, vikiwemo vidogo, vya kati na vikubwa, lakini ni vinane pekee vilivyo katika kundi la viwanda vikubwa.

Kufikia mwaka 2025/2026, Tanzania ilikuwa na idadi ya ng'ombe inayokadiriwa kufikia milioni 39.24, ikiwa ni ongezeko la asilimia 3.4 kutoka takwimu zilizopita.

Tanzania ni nchi ya pili kwa idadi kubwa ya ng'ombe barani Afrika, ikionyesha umuhimu wa sekta ya mifugo kiuchumi.

 

CHANZO:TRT Afrika Swahili