Zhang Kequn alikamatwa mwezi Machi katika uwanja wa ndege wa JKIA akiwa na zaidi ya mchwa 2,200.
Mahakama ya Kenya siku ya Jumatano, Aprili 15, iliamuru raia huyo wa China aliyepatikana akijaribu kusafirisha mchwa hai nje ya nchi kinyume cha sheria kulipa faini ya shilingi milioni 1 (dola 7,746) na kutumikia kifungo cha miezi 12 gerezani.
Jaji katika kesi hiyo alisema adhabu kali ilihitajika ili iwe fundisho kwa wengine, kufuatia kuongezeka kwa visa kama hivyo nchini Kenya.
Wadudu hao mara nyingi husafirishwa China, Marekani na Ulaya, ambako hufugwa majumbani na thamani ya mdudu mmoja inakaribia dola 100 za Marekani.
Usafirishaji wa mchwa ulivuta hisia kubwa za vyombo vya habari mwaka jana baada ya vijana wawili kutoka Ubelgiji kukamatwa wakiwa na karibu mchwa 5,000, na kutozwa faini ya takribani dola 7,700.












