| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Misri, Qatar wasisitiza utekelezaji wa makubaliano ya awamu ya kwanza ya kusitisha mapigano Gaza
Wito huo unakuja huku makundi ya Palestina na wapatanishi walifanya mazungumzo jijini Cairo kwa lengo la kuelekea hatua nyingine ya makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza huku Israel ikiendelea na ukiukaji.
Misri, Qatar wasisitiza utekelezaji wa makubaliano ya awamu ya kwanza ya kusitisha mapigano Gaza
Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri Badr Abdelatty na Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar Mohammed bin Abdulrahman Al Thani. / Wengine

Misri na Qatar wamesisitiza umuhimu wa kutekeleza awamu ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza.

Mpango wa awamu ya kwanza unajumuisha kusitishwa mapigano na kubadilishana wafungwa kati ya Israel na makundi ya Palestina.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri Badr Abdelatty na Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar Mohammed bin Abdulrahman Al Thani pia walijadili “njia ya kuimarisha ushirikiano kati ya Misri na Qatar katika maeneo mbalimbali, na kukubaliana kuendeleza uratibu wa masuala ya kadhaa ya kikanda kwa njia ambazo zinazingatia maslahi ya pamoja na kuhakikisha usalama wa mataifa ya Kiarabu," Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri ilisema katika taarifa.

Majadiliano hayo pia yaliangazia yanayojiri katika kanda, huku pande zote mbili zikisisitiza “umuhimu wa utekelezaji wa masharti ya mpango wa awamu ya kwanza wa Rais wa Marekani (Donald) Trump (kumaliza vita Gaza)," wizara hiyo ilisema.

Mpango wa masharti 20

Trump alitangaza mpango wa masharti 20 mwezi Septemba akieleza kuhusu utaratibu wa kusitisha mapigano ambao unajumuisha kuwaachia huru mateka wa Israel, Israel kuondoka Gaza, kuundwa kwa uongozi wa wataalamu na kupelekwa kwa kikosi cha amani cha kimataifa, pamoja na wito kwa Hamas kusalimisha silaha.

Hata hivyo, Israel imeendelea kukiuka makubaliano hayo karibu kila siku.

Makundi ya Palestina na wapatanishi walifanya mazungumzo jijini Cairo kwa lengo la kuelekea hatua nyingine ya makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza huku Israel ikiendelea na ukiukaji

Katika awamu ya pili, Israel inatarajiwa kuondoka katika maeneo hayo, huku kikosi cha amani cha kimataifa kikianza majukumu ya kuhakikisha usalama, ikiwemo kufikisha misaada kwa watu na vifaa vya ujenzi upya.

Mauaji ya halaiki ya Israel huko Gaza tangu Oktoba 2023 yamewaua Wapalestina zaidi 73,000 na kuwajeruhi zaidi ya 173,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, kulingana na takwimu za Palestina.

Licha ya kusitishwa mapigano kuanza kutekelezwa Oktoba 10, 2025, jeshi la Israel limewaua Wapalestina wasiopungua 947 na kuwajeruhi 2,935 katika mashambulizi ya kila siku, kulingana na Wizara ya Afya ya Gaza.

CHANZO:AA