Tanzania yajiandaa na athari za mgogoro wa Mashariki ya Kati, yataka diplomasia itumike
Amesisitiza kuwa suluhisho la kudumu ni mazungumzo ya kidiplomasia ili kuepusha athari kubwa zaidi kwa uchumi wa dunia.
Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Gerson Msigwa, amesema athari za kupanda kwa bei ya mafuta zinatarajiwa kuonekana katika mataifa mengi duniani, si Tanzania pekee, kufuatia mvutano unaoendelea kati ya Iran, Israel na Marekani.
Amesisitiza kuwa suluhisho la kudumu ni mazungumzo ya kidiplomasia ili kuepusha athari kubwa zaidi kwa uchumi wa dunia.
Msigwa alikuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Mkoa wa Mwanza nchini humo ikiwa ni muendelezo wa utaoaji wa taarifa yake ya mara kwa mara kwa waandishi.
Akizungumzia mradi wa gesi asilia (LNG) kusini mwa Tanzania, Msigwa amesema serikali ipo kwenye hatua za mazungumzo zinazoendelea, ikilenga kuhakikisha rasilimali hiyo inanufaisha taifa kwa kiwango kikubwa.
Hata hivyo, ameeleza kuwa tarehe rasmi ya kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo bado haijatangazwa, huku taratibu mbalimbali zikiendelea kukamilishwa.
Aidha, serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali, ikiwemo maji, kwa lengo la kuboresha ustawi wa wananchi.