Congo: Rais Nguesso awania urais tena

Katika Uchaguzi Mkuu wa 15 Machi 2026 mgombea wa chama tawala cha Parti Congolais du Travail (PCT) ni Rais wa sasa Denis Sassou Nguesso, ambae anachuana na wagombea wengine sita.

By Coletta Wanjohi
Rais wa sasa wa Congo Denis Sassou Nguessoalianza uongozi mwaka1979 na baadaye akachuluia tena1997 / REUTERS

Jamhuri ya Congo inajiandaa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Machi 15, 2026.

Nchi hii inapakana na Angola, Cameroon, Jamhuri ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Gabon.

Katika Uchaguzi Mkuu, mgombea wa chama tawala cha Parti Congolais du Travail (PCT) ni Rais wa sasa Denis Sassou Nguesso, ambae anachuana na wagombea wengine sita.

Vyama viwili vya upinzani vimesusia kushiriki Uchaguzi Mkuu kwa madai kwamba mchakato huo hauna uwazi.

Akiwa na umri wa miaka 82, anataka kuchanguliwa kuongoza nchi hiyo kwa muhula wa tano mtawalia tangu arudi madarakani baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya 1993 na 1999.

Alichukua madaraka kwa mara ya kwanza mwaka 1979 chini ya mfumo wa chama kimoja.

Baada ya kushindwa katika uchaguzi wa 1992 wakati wa mfumo wa vyama vingi, aliibuka tena kwenye jukwaa la kisiasa mnamo 1997 kupitia mapinduzi na amekuwa akishinda katika kila uchaguzi tangu wakati huo.

Mnamo 2002 na 2009, alipata zaidi ya asilimia 85 na 78.61 ya kura za kitaifa mtawalia.

Kura hizo ziligubikwa na madai ya kutokuwa na usawa na haki.

Mwaka wa 2015 nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta ilifanya mageuzi ya kikatiba ambayo yaliondoa ukomo wa umri na vikwazo vya muda kwa wagombea wa urais.

Hivyo Sassou Nguesso aliendeleza utawala wake kupitia ushindi katika chaguzi za 2016 na 2021.

Upinzani ulipinga matokeo ya kila uchaguzi ambao alitangazwa mshindi.

Mabadiliko ya katiba pia yaliruhusu rais kuwa na mihula mitatu madarakani badala ya miwili.

Na ndio maana Sassou Nguesso sasa anawania muhula wake wa tatu na wa mwisho iwapo atashinda.

Rais mwenyewe ameanza kuzungumza kwa uwazi zaidi kuhusu urithi wa uongozi, akiwaambia wafuasi wachanga katika mkutano wake wa ufunguzi wa kampeni Februari 28 kwamba kizazi chake "kinaweka msingi" wa kuchukua uongozi.

Sassou ameahidi kuboresha miundombinu mipya, uwekezaji mkubwa katika kilimo na mseto wa kiuchumi.

Ahadi zake hata hivyo zinapingwa na baadhi ya wananchi wanaodai kwamba gharama ya maisha pamoja na ubora wa maisha imekuwa ni changamoto ya muda mrefu katika uongozi wake wa karibu miaka 42.