Ghana imeanza majadiliano na shirika la serikali la Urusi la nishati ya nyuklia Rosatom kuhusu mipango ya ujenzi wa kiwanda cha kwanza cha umeme wa nyuklia nchini humo, Rais John Dramani Mahama ametangaza.
Mahama ametangaza hayo siku ya Alhamisi wakati akihutubia Kongamano la Tatu la Urusi na Afrika jijini Moscow, ambapo alieleza umuhimu wa upatikanaji wa umeme bila usumbufu na wa bei nafuu kusaidia katika ukuaji wa viwanda kwenye bara, Shirika la Habari la Ghana limeripoti.
Rais wa Ghana alieleza kuhusu kutopatikana kwa umeme wa kutosha kama moja ya vikwazo kwa maendeleo barani Afrika, akisema nishati ya nyuklia inaweza kusaidia kukabiliana na mahitaji ya umeme yanayoongezeka.
“Tumeanza majadiliano na Rosatom kuhusu kuanzisha kiwanda cha kwanza cha umeme wa nyuklia nchini Ghana,” Mahama alisema.
Kuwa na njia mbadala za nishati
Alisema Ghana inaangazia mkakati wa njia kadhaa za upatikanaji wa umeme ikiwemo nishati endelevu kwa maandalizi ya matumizi salama ya umeme wa nyuklia.
Tangazo limedhihirisha msingi wa ushirikiano wa muda mrefu wa nishati ya nyuklia kati ya Ghana na Urusi, ulioanza tangu mwaka 1964, wakati Muungano wa Sovieti ulipowapa Ghana kinu cha nyuklia cha megawati mbili kwa lengo la kufanya utafiti wa kisayansi.
Mahama amesema wanasayansi kadhaa wa nyuklia wa Ghana walipata mafunzo yao ya kusimamia kinu hicho nchini Urusi.




















