Soko la halal lenye thamani ya dola trilioni 7 laimarisha mustakabali wa sekta hio: Rais wa Uturuki

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, amesema kuwa sekta ya halal duniani imekua hadi kufikia thamani ya dola trilioni 7, na kwamba watu wengi ulimwenguni sasa wanapendelea bidhaa za halal.

By
Mkutano wa Maonesho ya Halal ulianza kwa wakati mmoja Jumatano huko Istanbul. / AA

Ukweli kwamba bidhaa na huduma halali hutolewa kwa watumiaji ambao huweka umuhimu katika usafi, afya, na wanaojali kidini, na kufikia karibu watu bilioni mbili ulimwenguni kote, huongeza imani katika mustakabali wa sekta hiyo, aliongeza.

Katika ujumbe wake kwa hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Dunia wa bidhaa za Halal uliofanyika Jumatano, Erdogan aliangazia kuwa mkutano huo uliwakaribisha wageni 50,000 kutoka nchi 50 na zaidi ya kampuni 500 mwaka uliopita, akiongeza kuwa anaamini idadi hiyo itaongezeka mwaka huu.

Amesema mkutano huo ndio tukio kubwa zaidi katika soko la kimataifa la halal na utakuwa na athari kubwa katika kukuza sekta hiyo.

Mkutano wa Dunia wa Bidhaa za Halal na Maonesho ya Halal yalianza kwa pamoja Jumatano mjini Istanbul, yakiwaleta wadau wa sekta hii chini ya kaulimbiu kuu ya “Kuimarisha Sekta ya Halal kupitia Ubunifu na Ubora.”

Toleo la 11 la mkutano huo na maonesho linatarajiwa kuendelea kuanzia Novemba 26 hadi 29, chini ya usimamizi wa Ofisi ya Rais wa Uturuki, kwa ushirikiano na Shirika la Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) pamoja na taasisi kadhaa zikiwemo Wizara ya Biashara ya Uturuki na Wakala wa Uidhinishaji wa Bidhaa za Halal.

Nchi za Kiislamu zinapaswa kuonyesha mshikamano zaidi

Waziri wa Biashara wa Uturuki, Omer Bolat, amesema dunia inapitia kipindi kigumu, ulinzi wa masoko unaongezeka, na ushuru wa forodha unapanda.

Amesisitiza kuwa lengo la ulimwengu wa Kiislamu ni kuhakikisha nchi za Kiislamu zinaonyesha mshikamano zaidi katika kipindi hiki, kuimarisha maendeleo ya kiuchumi, na kuongeza kiwango cha biashara baina yao.

Akigusia janga la kibinadamu huko Gaza, alisema: "Ninatoa salamu kwa ndugu zetu wa Gaza na Palestina, ambako karibu ndugu zetu 70,000 Wapalestina wamepoteza maisha katika kipindi cha zaidi ya miaka miwili kutokana na mashambulizi makali na mauaji ya kikatili ya Israel. Walifanya historia kwa kuonyesha ukaidi madhubuti dhidi ya mauaji ya Israel kwa niaba ya Umma wa Kiislamu wenye watu bilioni mbili. Tunatumai kwa dhati kuanza kwa enzi ya amani, yenye uthabiti, ujenzi upya na uanzishaji wa misaada Gaza na Palestina, sambamba na makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa nchini Misri."

Biashara ya halal yaweka mbele uaminifu, ubora, maadili na afya ya binadamu

Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Uturuki ya Kaskazini mwa Cyprus (TRNC), Fikri Ataoglu, amesema biashara ya halal si nguvu ya kiuchumi pekee bali pia ni jukwaa muhimu la kidiplomasia linalounganisha maeneo mbalimbali ya dunia, kuongeza hadhi ya nchi na kuwaleta watu pamoja.

Amesema Maonesho ya Halal yamekua kuwa kitovu muhimu kinachojumuisha uwezo wa uzalishaji wa ulimwengu wa Kiislamu, mtazamo wa biashara, na malengo ya pamoja.

Ameeleza kuwa biashara ya halal huweka kipaumbele katika uaminifu, ubora, maadili, uwajibikaji wa ufuatiliaji wa bidhaa na afya ya mwanadamu, akiongeza: “Kila moja ya thamani hizi pia huongeza hadhi ya chapa ya nchi.”

"Kupanda kwa umaarufu wa bidhaa za halal katika masoko ya kimataifa hakutengenezi tu fursa mpya za biashara, bali pia kunaimarisha taswira ya nchi, kufungua milango ya utambulisho wa kitamaduni, na kuwa dirisha linalowafanya watu kuifahamu nchi kwa mara ya kwanza."