Papa Leo XIV kutembelea bara la Afrika
Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani, analenga kuanza ziara yake hiyo kwa kuitembelea kwanza nchi ya Algeria.
Akikamilisha ziara yake ya kwanza kimataifa siku ya Jumanne, Papa Leo XIV ameonesha nia ya kuitembelea Algeria, ikiwa ni ziara yake ya kwanza barani Afrika, kama kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani.
"Natumai kuitembelea Afrika," alisema Baba Mtakatifu huyo wakati wa mkutano na waandishi wa habari ndani ya ndege yake, akitokea kwenye ziara ya siku sita ya kuitembelea Uturuki na kisha Lebanon.
"Binafsi, natumai nitafika Algeria na kutembelea maeneo muhimu ya Mtakatifu Augustino,” alisema Papa Leo XIV, akimzungumzia mtakatifu huyo wa karne ya tano, ambaye anatokea Afrika ya Kaskazini.
Papa Leo XIV, ambaye alichaguliwa kuongoza kanisa hilo lenye waumini bilioni 1.4 duniani, mwezi Mei mwaka huu, anatokea shirika la Waagustino, lililoanzishwa karne ya 13, likiwa na wafuasi wapatao 3,000 katika mataifa 50 ulimwenguni.
Kulingana na Papa Leo XIV, ziara ya nchini Algeria, itafungua milango ya majadiliano na kuwaleta pamoja Wakristo na Waislamu duniani.
"Mtakatifu Augustino ana nafasi kubwa nchini Algeria," alisema.