Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limewaomba radhi watumiaji wa huduma za umeme nchini humo, kufuatia hitilafu iliyojitokeza kwenye mfumo wa Gridi ya Umeme ya Taifa, Juni 27, 2026.
Hali hiyo, ilisababisha kukosekana kwa huduma ya umeme katika maeneo mbalimbali nchini humo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Lazaro Twange, alisema kuwa uchunguzi wa awali uliofanywa wakati wa hatua za kurejesha huduma ulibaini kuwa kutoka kwa gridi kulisababishwa na hitilafu zilizojitokeza kwa wakati mmoja katika njia tatu za usafirishaji wa umeme pamoja na mashine moja ya kuzalisha umeme.
"Tunatambua usumbufu uliowakumba wananchi na wateja wetu kutokana na hitilafu hii, na tunawaomba radhi. Wataalamu wetu walifanya kazi usiku na mchana kuhakikisha huduma ya umeme inarejea kwa haraka na kwa usalama," Twange alisema.
Kulingana na Twange, licha ya uwepo wa tukio hilo, hali ya uzalishaji wa umeme nchini inaendelea kuwa imara, ambapo uwezo wa uzalishaji umefikia takribani megawati 4,400 kiwango ambacho kinatosheleza mahitaji ya sasa ya nchi.
"Tunawaomba wananchi waendelee kuwa na imani na TANESCO. Sambamba na kuendelea kuimarisha uzalishaji wa umeme, tunawekeza katika kuboresha miundombinu ya Gridi ya Taifa ili kuongeza uthabiti wa mfumo na kupunguza uwezekano wa kujitokeza kwa hitilafu za aina za aina hii siku za usoni. Dhamira yetu ni kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma ya umeme ya uhakika, salama na endelevu," aliongeza.
Gridi ya Umeme ya Taifa ni mfumo mmoja unaounganisha miundombinu ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme, hivyo hitilafu kubwa inapotokea katika sehemu mojawapo ya mfumo huo inaweza kuathiri utendaji wa gridi nzima na kusababisha kukosekana kwa huduma ya umeme katika maeneo mengi kwa wakati mmoja.
















