Mtoto wa Waziri Mkuu wa zamani wa DRC Patrice Emery Lumumba afariki dunia

Kifo chake kinakuja wakati kesi za mauaji ya Patrice Lumumba zikiwa bado zinaendelea nchini Ubelgiji.

By
Roland-Gilbert Okito Lumumba akiwa amesimama kando ya picha ya baba yake./Picha:Wengine

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Félix-Antoine Tshisekedi ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Patrice Emery Lumumba, kufuatia kifo cha mtoto wa kiongozi huyo, Roland-Gilbert Okito Lumumba.

Roland-Gilbert, ambaye ni mtoto wa mwisho wa Patrice Emery Lumumba, alifariki dunia jijini Kinshasa, akiwa na umri wa miaka 67, baada ya kuugua.

Mtaalamu huyo wa usanifu wa majengo ambaye pia, amewahi kuhudumu kama mbunge wa zamani nchini DRC, atakumbukwa kwa jitihada zake za kutafuta ukweli kuhusu kifo cha baba yake, Patrice Lumumba, ambaye aliuawa mwaka wa 1961.

Kifo chake kinakuja wakati kesi za mauaji ya Patrice Lumumba zikiwa bado zinaendelea nchini Ubelgiji.

Baba yake alikuwa ni Waziri Mkuu wa DRC, miezi michache baada ya nchi hiyo (wakati huo ikiitwa Zaire) kabla ya kuondolewa madarakani na Wabelgiji mwaka 1961.

Mwaka 2002, Ubelgiji iliomba msamaha kwa kushiriki mauaji ya kiongozi huyo wa zamani, na miaka 20 baadaye, iliirudishia familia yake, linalosadikiwa kuwa ni jino la Patrice Lumumba mwenyewe.