| Swahili
ULIMWENGU
2 dk kusoma
Bunge la Yemen lawatangaza wapiganaji wa Houthi kuwa kundi la Kigaidi
Muswada huo, ulioungwa mkono na wabunge wote walioshiriki katika upigaji kura, unakataza kufadhili, kulipatia silaha au kusaidia shughuli za kundi hilo.
Bunge la Yemen lawatangaza wapiganaji wa Houthi kuwa kundi la Kigaidi
Bunge limesema kupitishwa kwa muswada huo ni wajibu wa kitaifa na kikatiba, likizitaka juhudi za kukomesha ufadhili wa kundi hilo ziungwe mkono. / / Reuters

Bunge la Yemen limepitisha muswada unaolenga kulitambua kundi la wapiganaji wa Houthi kuwa kundi la kigaidi, hatua inayofungua njia ya kuchukuliwa kwa hatua kali za kisheria dhidi ya shughuli na vyanzo vya ufadhili wa kundi hilo, kwa mujibu wa shirika la habari la serikali la Saba.

Muswada huo, ulioungwa mkono na wabunge wote walioshiriki katika upigaji kura, unakataza kufadhili, kulipatia silaha au kusaidia shughuli za kundi hilo. Sasa unasubiri kuidhinishwa na Rashad al-Alimi, mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Rais, ili uweze kuanza kutekelezwa.

Uamuzi huo ulifikiwa Jumatatu, baada ya wabunge kufanya majadiliano kwa siku mbili na kutathmini mapendekezo ya kamati maalumu ya bunge. Kikao cha kupiga kura kilifanyika kwa njia ya video, huku wawakilishi wa serikali wakishiriki katika mchakato huo.

Muswada huo unahusu shughuli zote za Wahouthi, kuanzia uongozi wa kisiasa hadi mifumo yake ya kijeshi na kiraia. Pia unaainisha makosa mbalimbali yatakayochukuliwa kuwa ya jinai, yakiwemo kuteka taasisi za serikali, kuzingira miji na kuwanyima wakazi chakula, kushambulia raia na meli za kimataifa, pamoja na kutumia watoto katika vita.

Makosa mengine yaliyotajwa ni kutega mabomu ya ardhini, utekaji nyara na kuwashikilia watu katika mazingira ya kutoweka kwa lazima. Kwa baadhi ya makosa hayo, wahusika wanaweza kukabiliwa na adhabu ya hadi kifo.

Vilevile, sheria hiyo inapendekeza kufuatiliwa na kufungiwa kwa mali zinazohusishwa na kundi hilo. Inaweka pia msingi wa ushirikiano na mataifa mengine katika masuala ya mahakama, kubadilishana ushahidi na kulinda haki za waathiriwa.

Bunge limesema kupitishwa kwa muswada huo ni wajibu wa kitaifa na kikatiba, huku likizitaka nchi nyingine kuunga mkono juhudi za kukomesha ufadhili na usambazaji wa silaha kwa kundi hilo. Pia limetoa wito wa kuchukuliwa kwa hatua za kulinda usalama wa usafiri wa meli katika njia za kimataifa.

Kwa upande wao, wapiganaji wa kundi la Houthi hawakujibu kuhusu uamuzi huo kufikia wakati taarifa hiyo ilipotolewa.

Hatua ya bunge inafuatia uamuzi wa Baraza la Mawaziri la Yemen kuidhinisha rasimu ya muswada huo Oktoba 11 na kuiwasilisha bungeni.

Haya yanajiri wakati mapigano nchini Yemen yakiongezeka tangu Julai, baada ya kipindi cha utulivu wa kiasi kilichofuatia makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa kuanzia Aprili 2022.

Kundi la Wahouthi lilitwaa udhibiti wa mji mkuu Sanaa na maeneo mengine ya Yemen Septemba 2014, hatua iliyochochea kuongezeka kwa mzozo nchini humo. Mnamo Machi 2015, muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia uliingilia kati kwa lengo la kuisaidia serikali ya Yemen.

CHANZO:Anadolu Agency