Rais wa Urusi, Vladimir Putin, amemhakikishia mwenzake wa Marekani, Donald Trump, kwamba Urusi haina nia ya kuzishambulia nchi za Ulaya, kwa mujibu wa taarifa iliotoka Ikulu ya Kremlin.
Kauli hiyo imetolewa wakati viongozi hao wawili wakijadili namna ya kupata suluhu ya mzozo wa Ukraine katika mazungumzo ya simu yaliyoelezwa kuwa “ya wazi na ya dhati.”
Mazungumzo hayo yaliyofanyika siku ya Jumanne “yalidumu kwa saa moja, yalikuwa yenye tija, ya wazi na ya dhati,” Yuri Ushakov, msaidizi wa rais wa Urusi, aliwaambia waandishi wa habari. Aliongeza kuwa mazungumzo hayo yalikuwa “ya siri kabisa.”
Ushakov amesema Putin “alisisitiza kwamba hatuna kabisa mpango wowote wa kushambulia Ulaya.”
Marais hao pia walijadiliana kuhusu ziara za hivi karibuni jijini Moscow na Kyiv zilizofanywa na wajumbe maalumu wa Marekani, Steve Witkoff na Jared Kushner. Kwa mujibu wa Ushakov, juhudi zao za kuendeleza mazungumzo ya amani zilitathminiwa kwa mtazamo chanya.
“Kwa ujumla, ziara ya wawakilishi hao wa Marekani ilitathminiwa vyema,” Ushakov alisema.
‘Tathmini ya hali halisi’
Ushakov amesema Trump alisisitiza umuhimu wa kumaliza mapema mzozo wa Ukraine, jambo ambalo linaweza kufungua njia ya kurejeshwa kwa kiwango kikubwa kwa uhusiano kati ya Urusi na Marekani.
Kwa mujibu wa Ushakov, Putin alimpa Trump “tathmini ya hali halisi” kuhusu hali ilivyo kwenye uwanja wa vita. Viongozi hao pia walijadili hatua ambazo Marekani inaweza kuchukua kusaidia kumaliza mapigano kwa haraka zaidi.
Kwa mujibu wa Ushakov, marais hao walikubaliana pia kuendelea kushughulikia masuala ya kibinadamu, ikiwa ni pamoja na kubadilishana wafungwa, na kuendelea kuwasiliana.
Ushakov alisema viongozi hao pia walijadili “madai ya Ulaya kuhusu tishio kutoka Urusi,” ambayo alisema “yanatumika kuhalalisha kuendelea kuisaidia Ukraine na kuongeza matumizi ya kijeshi barani Ulaya.”
Witkoff na Kushner walikutana na Putin mjini Moscow siku ya Jumamosi, kabla ya kusafiri kwenda Kyiv siku iliyofuata kwa mazungumzo na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy.
Urusi ilieleza mkutano huo na Putin kuwa “wa kina, wa kujenga na wenye manufaa makubwa,” lakini hakuna mafanikio maalumu au makubaliano makubwa yaliyotangazwa.




















