Siku 100 za Rais Samia: Ahadi, makovu ya uchaguzi na maisha halisi ya mwananchi
Lakini kwa baadhi ya wananchi, kauli hiyo haijatafsiriwa katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku.
Wiki hii, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametimiza siku 100 tangu ashike hatamu ya uongozi wa Tanzania, taifa la Afrika Mashariki lililobarikiwa rasilimali lukuki kama madini, mito na maziwa lakini vile vile rasilimali watu.
Hata hivyo, wabobezi wa masuala ya kisiasa wanakiri kwamba, siku hizi 100 zimeacha taswira mbili tofauti—taswira ya matumaini kwa upande wa serikali, na taswira ya sintofahamu kwa upande wa wananchi.
Kipindi hiki kinakuja baada ya kumbukumbu nzito za matukio ya Oktoba 29 kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu.
Akizungumza na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao, Rais Samia alisisitiza juu ya usalama wa nchi na umoja wa kitaifa, akieleza kuwa licha ya yaliyotokea, taifa bado limesimama pamoja.
Lakini kwa baadhi ya wananchi, kauli hiyo haijatafsiriwa katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku.
Zakaria Daniel, dereva wa pikipiki ya magurudumu matatu maarufu bajaji, anasema siku 100 hazijabeba maana yoyote kwake. Anahisi bado kuna ubaguzi katika upatikanaji wa huduma muhimu, hususan katika sekta ya afya.
“Ukienda hospitali, kabla ya kuhudumiwa wanaangalia mavazi na muonekano wako,” alisema Zakaria.
Anaongeza kuwa licha ya uzinduzi wa Bima ya Afya kwa Wote, utekelezaji wake bado unatiliwa shaka, huku changamoto za upatikanaji wa huduma za afya zikionekana kuongezeka badala ya kupungua.
Kwa upande wake, Lodom Mwakyambo anasema siku 100 zimeenda vyema kwa mtazamo wa jumla, lakini tatizo la ajira kwa vijana bado ni mwiba mkubwa. Kwa mujibu wake, vijana wengi waliosomea taaluma mbalimbali wamejikuta wakihangaika mitaani bila ajira.
Anasema licha ya kuanzishwa kwa Wizara ya Vijana, changamoto ya mikopo na uwezeshaji kwa vijana bado haijapatiwa ufumbuzi wa vitendo.
Aidha, anasisitiza umuhimu wa kukamilishwa kwa mchakato wa Katiba Mpya uliyoahidiwa katika awamu ya pili ya uongozi, ili kuwapa wananchi nafasi ya kweli ya kuchagua viongozi wanaowataka.
Peter Daniel, naye kijana, anakiri kuwa mambo mengi yametokea ndani ya siku 100, lakini utekelezaji wa ahadi kwa vijana bado ni ndoto.
“Huku chini bado hatujafikiwa. Wanaonufaika ni wale wachache waliopata umaarufu,” alisema.
Wakati wananchi wakitoa sauti zao, mawaziri wa serikali wameendelea kueleza mafanikio na vipaumbele vilivyotekelezwa ndani ya siku 100 za Rais Samia, wakisisitiza kuwa msingi wa maendeleo ya muda mrefu umewekwa.
Siku 100 zinaweza kuonekana nzuri kwenye hotuba na ripoti za serikali, lakini kwa baadhi ya mwananchi wa kawaida, bado wanataka serikali ifanye zaidi.