Balozi wa Iran nchini Lebanon atimuliwa

Lebanon imesema hatua hiyo ilitokana na "ukiukwaji wa Iram wa kanuni na itifaki za kidiplomasia" kati ya nchi hizo mbili.

By
Mwanga wa mlipuko unaonekana wakati wa shambulio la Israel uliolenga jengo huko Beirut, Machi 23, 2026. / / AP

Serikali ya Lebanon imetangaza kumfukuza balozi wa Iran nchini humo baada ya kumtangaza rasmi kuwa mtu asiyekaribishwa nchini (persona non grata), hatua inayodhihirisha kuongezeka kwa mvutano wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili.

Katika taarifa rasmi, Wizara ya Mambo ya Nje ya Lebanon imesema balozi wa Iran, Mohammad Reza Shibani, anatakiwa kuondoka nchini humo ifikapo tarehe 29 Machi. Hatua hiyo imechukuliwa kutokana na kile ilichoelezwa kuwa ni ukiukwaji wa misingi na taratibu za kidiplomasia unaofanywa na Iran.

Wizara hiyo pia imetangaza kumrejesha balozi wake nchini Iran, Ahmad Sweidan, kwa mashauriano, hatua inayotumika mara nyingi kama ishara ya kutoridhika katika mahusiano ya kidiplomasia.

Awali, tarehe 5 Machi, serikali ya Lebanon ilikuwa imeagiza vyombo vya usalama kuwafuatilia na kuwakamata wanachama wowote wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC) wanaofanya shughuli ndani ya nchi hiyo.

Mwaka uliopita, Rais wa Lebanon, Joseph Aoun, aliionya Iran akisisitiza kuwa hakuna kundi lolote ndani ya Lebanon linaloruhusiwa kubeba silaha au kutegemea msaada kutoka nje ya nchi.

Wakati huo huo, hali ya usalama nchini Lebanon imeendelea kuwa tete kufuatia mashambulizi ya Israel ambayo yamehusisha mashambulizi ya anga pamoja na operesheni ya kijeshi ya ardhini kusini mwa nchi hiyo tangu tarehe 2 Machi.

Kwa mujibu wa mamlaka za Lebanon, watu wasiopungua 1,039 wameuawa na wengine 2,876 kujeruhiwa kutokana na mashambulizi hayo ya Israel.

Mvutano huu pia unahusishwa na operesheni ya pamoja ya kijeshi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, ambayo imesababisha vifo vya zaidi ya watu 1,340 tangu tarehe 28 Februari.

Kwa upande wake, Iran imejibu kwa kufanya mashambulizi ya droni na makombora yakilenga Israel pamoja na nchi nyingine kama Jordan, Iraq na baadhi ya mataifa ya Ghuba, ikisema inalenga vituo vya kijeshi vya Marekani.