| Swahili
ULIMWENGU
2 dk kusoma
Iran kuzindua bomu lake kubwa zaidi “father of all bombs”
Msemaji wa Jeshi la Mapinduzi ya Iran (IRGC) hajatoa maelezo zaidi kuhusu silaha hiyo, siku chache baada ya Rais Donald Trump kudokeza uwezekano wa kutumia bomu la Marekani linalojulikana kama “mother of all bombs” dhidi ya Iran.
Iran kuzindua bomu lake kubwa zaidi “father of all bombs”
Makombora ya Iran yanaonyeshwa katika jumba la Makumbusho ya Jeshi la Anga la IRGC jijini Tehran. / / Reuters

Iran inajiandaa kuzindua silaha mpya ambayo imepewa jina la “father of all bombs,” kwa mujibu wa msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC).

“Tupo katika hatua ya kujiandaa kutangaza rasmi bomu kubwa zaidi ‘father of all bombs.’ Hii ni silaha mpya kwa adui,” alisema Hossein Mohebi siku ya Jumatano, katika taarifa zilizonukuliwa na shirika la habari la Young Journalists Club la Iran.

Hata hivyo, hakutoa maelezo zaidi kuhusu silaha hiyo.

Siku ya Ijumaa, Rais wa Marekani Donald Trump alidokeza uwezekano wa kutumia bomu lake kubwa zaidi lisilo la nyuklia (GBU-43/B Massive Ordnance Air Blast (MOAB), linalojulikana pia kama “mother of all bombs,” kulenga vituo vya nyuklia vya Iran.

Bomu hilo lina uzito wa takribani kilogramu 9,800 na ni miongoni mwa mabomu makubwa zaidi yasiyo ya nyuklia katika ghala la silaha la Marekani.

Bomu hilo lilitumika kwa mara ya kwanza Aprili 2017, wakati wa muhula wa kwanza wa urais wa Trump, dhidi ya mahandaki yaliokuwa yakitumiwa na kundi la kigaidi la Daesh nchini Afghanistan.

Mohebi pia alisema kuwa akiba ya makombora ya Iran imeongezeka kwa mara 1.5 kufuatia vita vya siku 12 kati ya Iran na Israel vilivyotokea Juni 2025. Hata hivyo, hakutoa takwimu mahususi kuthibitisha ongezeko hilo.

“Ubora wa makombora umeimarika kwa kiasi kikubwa, huku masafa yake, uwezo wake wa kusababisha uharibifu na usahihi wa kulenga malengo vikiongezeka,” aliongeza.

Marekani na Israel zilianzisha vita dhidi ya Iran Februari 28, huku Iran ikijibu kwa kufanya mashambulizi dhidi ya Israel na vituo vya kijeshi vya Marekani vilivyoko katika nchi za Ghuba.

Marekani na Iran zilitia saini hati ya makubaliano ya maelewano mwezi Juni, kisha zikaanza mazungumzo ambayo baadaye yalivunjika kutokana na kutokubaliana kuhusu uhuru wa usafiri wa meli na masuala ya usalama katika Mlango-Bahari wa Hormuz.

Mlango-Bahari huo ni njia muhimu ya kimkakati inayotumiwa kusafirisha nishati na bidhaa mbalimbali.

CHANZO:AA