Namna katiba ya Somalia itakavyoathiri maafisa wa ngazi za juu
Hii ni katiba ya kwanza ya katika kipindi cha karibu miongo minne, ana iliidhinishwa na mabunge yote mawili ya nchi hiyo tarehe 4 Machi, 2026.
Katiba mpya ya Somalia inatarajiwa kubadilisha muelekeo wa kisiasa wa nchi kukiwa na mabadiliko ya namna viongozi wa nchi wanavyochaguliwa.
Ni katiba ya kwanza ya Somalia katika kipindi cha karibu miongo minne, na iliidhinishwa na mabunge yote mawilli ya nchi hiyo siku ya Jumatano, tarahe 4 Machi, baada ya miezi kadhaa ya majadiliano.
Wabunge wamefanya mabadiliko makubwa katika katiba ya muda ya Somalia, ambayo nchi hiyo ilianza kutumia tangu 2012.
Kwa sasa, kwa mtu kugombea nafasi za juu, usiwe umeoa au umeolewa na raia wa kigeni, usiwe na uraia pacha, na wazazi wako wote wawili wawe ni Wasomali.
Kwa wale wenye uraia pacha na wanahitaji kugombea nafasi za kisiasa nchini, lazima wajivue uraia wa kigeni.
Mabadiliko hayo yanalenga yale ambao wengi wanataja kuwa nafasi “Tatu Kubwa”: Rais, Waziri Mkuu, na Maspika wa Mabunge yote mawili.
Ujumbe wa mabadiliko haya ni wazi — Taasisi za juu za maamuzi za Somalia lazima ziwe watiifu kwa taifa.
Hili ni muhimu kwa kuwa katika nyakati tofauti zilizopita, Somalia imekuwa na rais na waziri mkuu waliokuwa na uraia pacha.
Kuongezwa kwa muhula wa urais
Katiba hiyo mpya, iliyoandikwa kwa lugha ya Kisomali, imeongezwa muhula wa urais kutoka miaka minne hadi miaka mitano lakini ikajumuisha kuwa itakuwa mihula miwili tu kwa rais.
Hata hivyo, rais anapomaliza mihula yake miwili, moja kwa moja anakuwa mjumbe wa Bunge la Juu kwa umri wote wa uhai wao.
Kulingana na sheria mpya, wagombea wa urais na uwaziri mkuu wanatakiwa kuwa na umri usiopungua miaka 40.
Suala kuu ni, viongozi hawa watachaguliwa vipi? kwa miongo kadhaa, Somalia imekuwa na mfumo usio wa moja kwa moja, wa kikoo ambapo wajumbe wanachagua wabunge, ambao baadaye wanamchagua rais wa nchi.
Katika mfumo huu mpya, Wabunge na Maseneta watachaguliwa moja kwa moja na wananchi katika hatua ya kuhakikisha kuwa kila mtu anashiriki katika upigaji kura.
Hata hivyo, Rais wa Somalia ataendelea kuchaguliwa na mabunge yote mawili.
‘Hatua ya kihistoria’
Katiba hiyo mpya pia inatambua rasmi serikali tatu – Serikali Kuu, Serikali ya Majimbo, na Serikali za Mitaa.
Hii ni katiba ya kwanza ya Somalia tangu kuporomoka kwa taifa hilo 1991 kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Itachukua nafasi ya katiba ya sasa ya Muda iliyokuwepo tangu 2012.
Spika wa Bunge, Aden Mohamed Nur Madoobe, ambaye alisimamia kikao cha pamoja kilichoidhinisha katiba hiyo, alieleza ‘’katiba hiyo kuwa ya kihistoria.’’
Hata hivyo, baadhi ya wanasiasa wa upinzani wameeleza wasiwasi wao kuhusu kutojumuishwa kila mtu katika mchakato huo.
Rais Hassan Sheikh Mohamud ana siku 30 kusaini katiba hiyo kuwa sheria kabla haijachapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali ili ianze kutekelezwa.