| Swahili
AFRIKA
3 dk kusoma
Putin anaunga mkono juhudi za Afrika za kutaka mageuzi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Rais wa Urusi pia anatoa wito wa kufanyiwa marekebisho kwa IMF, Benki ya Dunia na WTO ili kuendana na hali halisi ya uchumi wa dunia inayobadilika.
Putin anaunga mkono juhudi za Afrika za kutaka mageuzi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Putin amesema BRICS Unakabiliwa na upinzani kutoka kwa wale waliozoea kufikiri kwa mtazamo wa kikoloni -- kuigawanya dunia

Rais wa Urusi Vladimir Putin siku ya Jumamosi alitoa wito wa kupanuliwa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili kuongeza uwakilishi wa nchi za Afrika, Asia na Amerika ya Kusini.

Umoja wa Afrika umekuwa ukishinikiza kuwepo kwa uwakilishi mkubwa zaidi wa Afrika katika taasisi za kimataifa. Bara hilo linachangia zaidi ya robo ya wanachama wa Umoja wa Mataifa lakini halina kiti cha kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja huo.

Akihutubia mkutano wa 18 wa kilele wa BRICS katika mji mkuu wa India, New Delhi, Putin alisema Urusi inatilia maanani sana suala la kudumisha na kuimarisha nafasi muhimu ya Umoja wa Mataifa katika masuala ya kimataifa, na inaamini kuwa wanachama wa BRICS wanapaswa kuendelea kushirikiana ili kuboresha ufanisi wa shirika hilo.

"Bila shaka, kupanua Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa - hasa kwa kuongeza uwakilishi wa nchi za Asia, Afrika, na Amerika ya Kusini - kungechangia kufikiwa kwa lengo hili," alisema Putin, kulingana na taarifa rasmi iliyotolewa na Kremlin.

Kukabiliana na hali halisi

Putin pia alisema kuna "hitaji la muda mrefu" la kuboresha taasisi za kimataifa za kiuchumi kama vile Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Benki ya Dunia na Shirika la Biashara Duniani (WTO), ambazo alisema zinapambana kukabiliana na "hali halisi ya kisiasa na kiuchumi" ya sasa.

Alisema IMF, WTO na Benki ya Dunia zimesalia kuwa njia muhimu za majadiliano kati ya mataifa yenye uchumi mkubwa duniani, na akatoa wito wa kuwepo kwa uratibu imara zaidi kati ya nchi za BRICS ndani ya taasisi hizo.

Akizungumzia kundi la BRICS, Putin alisema kuwa nchi wanachama zina uwezo mkubwa wa kiakili na kiteknolojia, akielezea sifa hizo kama faida kubwa kwa kundi hilo.

Alisema BRICS "imejiimarisha ipasavyo miongoni mwa vituo muhimu vya utawala wa kimataifa," akisisitiza kuwa mwenendo wa siasa za kimataifa, usalama, ushirikiano wa kiuchumi na masuala ya kibinadamu unazidi kutegemea maamuzi ya pamoja ya nchi wanachama wake.

Kuimarisha ushirikiano wa pande nyingi


Putin alisema kuwa katika kipindi hiki ambacho mfumo wa dunia wenye nguvu nyingi (multipolar) unaibuka, nchi za BRICS zinapaswa kushirikiana ili kuimarisha ushirikiano wa pande nyingi, kuhusisha nchi zaidi katika utawala wa kimataifa na kuongeza ushiriki wao katika taasisi muhimu za kimataifa.

"Hata hivyo, mchakato wa kuundwa kwa dunia yenye nguvu nyingi haukosi changamoto -- sote tunaweza kuona hilo. Unakabiliwa na upinzani kutoka kwa wale waliozoea kufikiri kwa mtazamo wa kikoloni -- kuigawanya dunia katika 'bustani inayostawi' na ya mwituni na kuishi kwa kutegemea rasilimali za wengine," alisema.

"Hawako tayari kukubali uhalisia unaobadilika na wanajitahidi kwa kila njia kudhibiti washindani wao wanaozidi kuimarika," Putin aliongeza, akibainisha kuwa mbinu hizo ni pamoja na vita vya ushuru wa forodha, vikwazo na matumizi ya "nguvu ya mabavu."

CHANZO:TRT Afrika and agencies