Watu wasiopungua 15 wauawa katika mashambulizi kijijini jimbo la Kebbi la Nigeria
Mashambulizi hayo yalitokea katika wilaya ya Shanga jimbo la Kebbi, yakilenga vijiji vya Gebe, Kawara, Kalkami na maeneo mengine ya karibu, polisi wamesema.
Magaidi wamewaua watu wasiopungua 15 katika mashambulizi kadhaa kwenye vijiji kaskazini magharibi mwa Nigeria, wakazi wa eneo hilo walielezea AFP siku ya Jumatatu.
Mashambulizi hayo yalitokea katika wilaya ya Shanga jimbo la Kebbi, yakilenga vijiji vya Gebe, Kawara, Kalkami na maeneo ya karibu, msemaji wa polisi jimbo la Kebbi Bashir Usman aliiambia AFP.
Pamoja na kuwa polisi haikueleza kuhusu idadi ya waliouawa, wakazi kutoka vijiji viwili wanasema huenda watu waliouawa si chini ya 15.
Usman Yahaya, mkazi wa Kalkami ambaye alikimbia mashambulizi hayo, anasema magaidi hao walikuwa wamevuka kutoka Jimbo la Niger.
"Walianza kuwafyatulia risasi watu wetu katika kijiji cha Kalkami, na kuchoma nyumba moto," alisema, akiongeza kuwa: "Waliwaua watu wasiopungua 10."
Malam Dan Tani Muhammad, mkazi wa kijiji kingine kilichoshambuliwa cha Kawara, anasema magaidi walifika huko Jumatatu asubuhi na kuwaua watu watano, pamoja na kuchoma nyumba.
Jimbo la Kebbi liko katika mpaka wa Nigeria na Benin na Niger na tangu 2025 limekuwa likikabiliwa na idadi kubwa ya mashambulizi ya magaidi.
Shirika linalofuatilia masuala ya migogoro ACLED linasema kumekuwa na ongezeko la mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa na makundi yenye ushirikiano na Al Qaeda na Daesh.