Imepita miaka 58 tangu Rais wa wakati huo wa Somalia, Aden Abdulle Osman, alipokubali kushindwa katika uchaguzi na kukabidhi madaraka kwa Abdirashid Ali Sharmarke, tukio linalotambuliwa kama makabidhiano ya kwanza ya madaraka kwa njia ya amani barani Afrika.
Tarehe 25 Disemba, mwelekeo wa kidemokrasia wa Mogadishu unapitia mabadiliko makubwa, kwa kufanyika kwa uchaguzi wa kwanza ambapo wananchi wameshiriki katika mchakato wa kupiga kura. Tukio hili linakuja wakati muhula wa Rais Hassan Sheikh Mohamud ukikaribia kumalizika Mei 2026, na wabunge wakimaliza muhula wao mwezi mmoja kabla.
Hatua hii ya kihistoria ya ambapo wananchi wanashiriki uchaguzi kwa mara ya kwanza baada ya karibu miongo sita—inaashiria mwanzo mpya. Tangu 2012 wabunge pekee ndio walikuwa wakipiga kura ya kumchagua rais, hii ni baada ya nchi hiyo kusambaratika kwa zaidi ya miaka 30.
Hata hivyo, hatua hii imekumbwa na changamoto nyingi, hasa tishio la upinzani kuanzisha “mchakato mbadala wa uchaguzi” huku wakishinikiza mazungumzo mapana kuhusu mwelekeo wa demokrasia ya nchi.
Changamoto zinazotokana na historia ya Somalia
Safari ya Somalia kufikia hatua hii ina mizizi yake katika makabidhiano ya madaraka kwa njia amani ya mwaka 1967 uliofanywa na Rais wa zamani Abdulle Osman. Hata hivyo, yaliyotokea katika kipindi kilichofuata pia yamechangia hali ya sasa ya nchi.
Miaka miwili baada ya kuingia madarakani, Sharmarke aliuawa, jambo lililofungua njia ya mapinduzi ya kijeshi yaliyosimamisha maendeleo ya kidemokrasia kwa miongo kadhaa. Uchaguzi wa chama kimoja uliodhibitiwa wa mwaka 1979 na 1984 ulikuwa ni matukio ya mpito tu, si juhudi za dhati za kurejesha demokrasia.
Ni miaka 13 tu iliyopita ambapo Somalia ilifanya uchaguzi wake wa kwanza wa maana tangu kipindi hicho cha misukosuko. Mchakato huo ulihusisha Bunge lililochaguliwa na wazee wa kimila, na kuashiria mwanzo wa juhudi za kuimarisha mfumo wa uchaguzi usio washirikisha wanachi.
Uchaguzi wa 2016 ulitofautiana na ule wa 2012, ulihusisha wajumbe 14,025 waliowachagua wabunge. Kufikia 2022, idadi ya wajumbe iliongezeka zaidi.
Katika mfumo huu, wabunge 275 pamoja na wajumbe 54 kutoka seneti wamchagua Rais.
Mchakato huu unaongozwa na taratibu kali. Makabila huwasilisha orodha ya wajumbe wao kwa Tume Huru ya Uchaguzi, pamoja na kusajiliwa kwa wazee 135 wenye jukumu la kuwachagua wabunge.
Kila nafasi lazima iwe na wagombea wasiopungua wawili. Uchaguzi wa wabunge hufanyika ndani ya tawala za kikanda, isipokuwa kwa wale wanaowakilisha Somaliland na Banadir, ambao hufanyika Mogadishu.
Baada ya majimbo ya shirikisho na makabila kukamilisha wawakilishi wao, orodha huthibitishwa na kupelekwa mji mkuu. Baada ya uchaguzi kukamilika, Rais mteule humteua Waziri Mkuu ndani ya siku 30, naye hupewa mwezi mmoja kuunda serikali.
Mchakato wa upigaji kura
Mabadiliko ya Somalia kutoka mfumo wa zamani wa upigaji kura yalianza Aprili 2025, wakati Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi na Mipaka (INEBC) ilipoanzisha mchakato wa usajili wa wapiga kura Mogadishu. Zaidi ya raia 900,000 walijiandikisha kupiga kura ndani ya muda uliowekwa.
Muundo wa wapiga kura unatoa picha ya kuvutia: takriban 94% ya wapiga kura waliosajiliwa Mogadishu wako chini ya umri wa miaka 44, huku 63% wakiwa wanaume. Idadi ya wapiga kura waliosajiliwa pia ndiyo kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya mji mkuu.
Kuongezeka huku kwa ushiriki wa raia kunakwenda sambamba na ushindani mkali wa kisiasa, ambapo vyama 20 vya siasa vina wagombea 1,600 kuwania viti 390.
Mamlaka zimefungua vituo 510 vya kupiga kura katika mji mkuu kwa ajili ya uchaguzi wa Disemba 25. Waangalizi wa uchaguzi wameteuliwa katika kila kituo, na takriban waandishi wa habari 100 wamepewa vibali vya kutoa taarifa za uchaguzi huu wa kihistoria.
“Tuko tayari kusimamia uchaguzi na tuna imani kuwa mchakato utafanikiwa. Kura hii inalenga kuwapa wananchi wa Somalia fursa ya kutumia haki yao ya kikatiba ya kuwachagua viongozi wao kwa uhuru,” alisema mwenyekiti wa INEBC, Abdikarim Ahmed Hassan.
“Ni heshima kwetu kupata imani ya umma na taasisi zote za serikali tunapofanya kazi pamoja kufanikisha uchaguzi huu wa kihistoria wa mtu mmoja kura moja.”
Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Somalia pia imetangaza kuwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Aden Adde Mogadishu utafungwa kwa saa 24 mnamo Disemba 25 ili kuwezesha mipango ya kiusalama na kiutendaji kwa uchaguzi wa eneo la Banadir.
Wasiwasi wa upinzani
Pamoja na hali ya matumaini yaliyopo, upinzani bado una mashaka kuhusu mchakato huu.
Rais wa zamani Mohamed Abdullahi Farmaajo, mwanzilishi wa Chama cha Kisiasa cha Tayo, alitoa taarifa akisema ni jambo la kusikitisha kuwa nchi bado haina “mwelekeo wa kisiasa uliokubaliwa na washikadau wote”.
“Ninapinga mpango wowote wa kuongeza muhula kwa njia isikuwa ya halali, uchaguzi unoendeshwa na kundi moja la kisiasa, inayonufaisha upande moja, au hatua zozote zinazoweza kuisukuma nchi kuelekea kuundwa kwa serikali mbili ,” alisema akiashiria utawala wa sasa.
Vyama vya upinzani vilikutana Kismayo hivi karibuni kuukosoa mchakato wa uchaguzi unaoendelea. Walisema unaendeshwa na “kundi moja la kisiasa” kwa njia inayokwepa Katiba ya Mpito na kukiuka haki za wananchi wa Banadir.
Hata hivyo, vyama hivyo vimeeleza utayari wao wa kufanya mazungumzo na Rais Mohamud. Walitoa wito wa kuundwa kwa tume ya uchaguzi yenye makubaliano ya pamoja na mchakato ulio “wazi, wa kuaminika na ulioboreshwa zaidi” kuliko ule wa 2022. Pia walisisitiza haja ya kuimarisha uwakilishi wa kikanda.
Ili kufanikisha hilo, upinzani umemtaka Rais kuwa na kikao na wadau wote wa kisiasa kabla ya Januari 20, 2026, ili kukubaliana juu ya mwelekeo wa mchakato wa uchaguzi kulingana na Kifungu cha 5 cha Katiba.
Kadri muda unavyokaribia, macho yote yanaelekezwa Mogadishu kuona iwapo kutakuwa na mabadiliko ya kisiasa.















