44 wauawa katika shambulio la kigaidi nchini Nigeria
Msemaji wa jeshi la polisi nchini Nigeria, Bashir Usman amesema kuwa matukio hayo, yamewalazimu kuanzisha operesheni ya kukabiliana na majingili na uhalifu mwingine katika maeneo hayo.
Watu wapatao 44 wameuawa katika mashambulizi yaliyofanyika katika jimbo la Kebbi, kaskazinimagharibi mwa Nigeria.
Kulingana na jeshi la polisi nchini humo, mashambulizi hayo yalilenga vijiji vilivyopo ndani ya eneo la mtaa wa Shanga, vikiwemo Gebe, Kalkami, Kawara, Kasoshi, Awaye, Tungar Rini, Binuwa na Dabe.
Matukio hayo yametokea siku moja baada ya afisa mwandamizi wa jeshi la nchi hiyo Brigedia I. A. Braimah, kuuawa pamoja na maofisa wengine baada ya kushambuliwa na wanamgambo wa Boko Harama katika jimbo la Borno.
Msemaji wa jeshi la polisi nchini Nigeria, Bashir Usman amesema kuwa matukio hayo, yamewalazimu kuanzisha operesheni ya kukabiliana na majingili na uhalifu mwingine katika maeneo hayo.
“Idadi kubwa ya polisi wamekita kambi katika maeneo yaliyoathirika kuhakikisha kuwa hali ya usalama inarejea mapema iwezekanavyo,” alisema Usman.
Kwa upande wake, kamishna wa polisi katika jimbo la Kebbi, Umar Hadejia, amewataka wakazi wa maeneo hayo kuwa waangalifu na kutoa taarifa kwa jeshi la polisi pindi wanapohisi kutokea kwa matokeo ya kihalifu.
Pia, amewataka viongozi wa jadi, dini pamoja na vijana kuunga mkono juhudi za kupambana na uhalifu katika jimbo hilo.