Mahakama Kuu nchini Kenya imetoa amri ya muda ya kuzuia Serikali kuanzisha, kuendesha, kuwezesha au kuruhusu kuanzishwa kwa kituo chochote cha karantini, au cha matibabu ya Ebola nchini Kenya chini ya makubaliano yanayopangwa kati ya Kenya na Marekani au serikali nyingine yoyote ya kigeni.
Mahakama pia imepiga marufuku kuruhusiwa kuingia kwa watu walioathiriwa au walioambukizwa Ebola chini ya mpango huo hadi pale ombi na kesi iliyowasilishwa mahakamani litakaposikilizwa na kuamuliwa.
Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia maswali yaliyoibuliwa kuhusu afya ya umma, uwazi katika mchakato huo, pamoja na masuala ya kikatiba na mamlaka ya taifa.
Kwa upande wake, akizungumzia suala hilo, Rais William Ruto alitetea mpango huo akisema kuwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha utayari wa Kenya katika kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza, na si tishio kwa usalama wa wananchi.

















