Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa jeshi la Marekani limefanya shambulio kubwa katika Kisiwa cha Kharg cha Iran na ametishia kushambulia miundombinu ya mafuta ya nchi hiyo iwapo Iran itazuia usafirishaji wa mafuta katika Mlango Bahari wa Hormuz.
"Kamandi Kuu ya Kati ya Marekani ilifanya mojawapo ya mashambulizi ya mabomu yenye nguvu zaidi katika historia ya Mashariki ya Kati na iliharibu kabisa kila ngome ya jeshi la Iran, katika Kisiwa cha Kharg," Trump alisema mapema Jumamosi katika mitandao ya kijamii.
"Nimeamua kutoangamiza miundombinu ya mafuta katika Kisiwa hicho. Hata hivyo, iwapo Iran, au mtu mwingine yeyote, atafanya chochote kuingilia upitishaji huru na salama wa meli zinazopitia Mlango Bahari wa Hormuz, nitafikiria upya mara moja."
Kisiwa muhimu
Marekani na Israel zimekuwa zikichukua tahadhari ya kisiwa hicho, lakini imearifiwa kwamba maafisa wa utawala wa Trump wamesema kuwa kuishambulia Kharg ilikuwa mojawapo ya hatua muhimu wakati vita vya Marekani na Israel katika Mashariki ya Kati vinaendelea.
Kisiwa hicho, kilicho takriban kilomita 30 kutoka pwani kuu ya Iran, kinashughulikia takriban asilimia 90 ya mauzo ya mafuta ghafi ya Iran, kwa mujibu wa taarifa ya hivi karibuni ya JP Morgan.
Eneo hilo ni takriban theluthi moja ya ukubwa wa Manhattan, na wataalamu walisema kwamba hatua yoyote dhidi yake ingesababisha athari za haraka.
Mashambulizi ya Iran karibu yamezuia usafiri wa meli kupitia Mlango Bahari wa Hormuz, ambao ni njia kuu ya kupitisha meli za mafuta ghafi ya dunia na gesi asilia iliyoyeyushwa, na pia yameathiri miundombinu ya mafuta katika mataifa mengine ya Ghuba.
Trump alisema Jeshi la Majini la Marekani litaanza kusindikiza meli za mafuta kupitia eneo hilo, "hivi karibuni" ili kurejesha usafirishaji wa mafuta, huku akijaribu kukabiliana na ongezeko la bei ya petroli nchini Marekani.
Kharg ilifanyiwa maboresho muhimu wakati ya upanuzi wa sekta ya mafuta ya Iran miaka ya 1960 na 1970, wakati sehemu kubwa ya pwani ya nchi hiyo ilikuwa na kina kifupi cha meli kubwa za mafuta (supertankers).













