Rais Tinubu wa Nigeria azuru Uingereza huku Afrika ikidai fidia kwa ukoloni

Ziara hiyo inajiri huku kukiwa na wito kwa mataifa ya Ulaya yalipe fidia kwa kile Umoja wa Afrika ulichoeleza kama "uhalifu dhidi ya ubinadamu" waliofanya wakati wa biashara ya utumwa na ukoloni.

By
Ziara ya rais Bola Tinubu ni ziara ya kwanza nchini Uingereza kufanywa na kiongozi wa Nigeria katika kipindi cha miaka 37. / / Others

Rais Bola Tinubu anazuru Uingereza kwa ziara ya kwanza ya kiserikali ya kiongozi wa Nigeria katika miongo kadhaa.

Akiondoka Abuja kuelekea London Jumanne, Machi 17, Rais Tinubu anaandamana na mkewe, Oluremi, pamoja na mawaziri kadhaa na maafisa wengine.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa rais wa Nigeria na Kasri ya Buckingham, Mfalme wa Uingereza, Mfalme Charles III, na mkewe, Malkia Camilla, watakuwa wenyeji wa rais wa Nigeria katika Windsor Castle, magharibi mwa London, kutoka 18 hadi 19 Machi.

Mshauri Maalumu wa Rais Tinubu kuhusu Habari na Mikakati, Bayo Onanuga, alisema kiongozi huyo wa Nigeria pia atafanya mkutano wa nchi mbili na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer, na makubaliano ya ‘’ kuhusu biashara, uwekezaji, ulinzi, na ushirikiano wa kitamaduni’’ yanatarajiwa kusainiwa.

Atashuhudia kusainiwa kwa mkataba wa ufadhili wa pauni milioni 746 kusaidia ‘’urekebishaji’’ wa vituo viwili vikubwa vya baharini vilivyoko Lagos.

Biashara ya kila mwaka kati ya nchi hizo mbili ilifikia pauni bilioni 8.1 - sawa na dola bilioni 11 mwaka 2025, ikiwa ni ongezeko la 11.4% la mwaka hadi mwaka.

Nigeria, koloni la zamani la Uingereza, ndiyo nchi yenye watu wengi zaidi na mojawapo ya nchi zenye uchumi mkubwa zaidi barani Afrika ikiwa na wakazi milioni 230.

Biashara ya watumwa na ukoloni

Ziara hiyo inajiri huku kukiwa na wito kwa mataifa ya Ulaya yalipe fidia kwa kile Umoja wa Afrika ulichoeleza kuwa ‘‘uhalifu dhidi ya ubinadamu’’ waliofanya wakati wa biashara ya utumwa na ukoloni.

Mahakama nchini Nigeria hivi karibuni iliamrisha Uingereza kulipa £420 milioni kwa familia za wachimbaji waliouawa mwaka 1949 na watawala wa kikoloni wa Uingereza, walipokuwa wakidai masharti bora ya kazi na mishahara yao ambayo haikuwalipwa.

Haijulikani kama Tinubu ataleta masuala hayo kwa mamlaka za Uingereza.

Ingawa Rais Tinubu alikuwa amewahi kutembelea London mara kadhaa, ikiwa ni pamoja na Septemba 2024 alipokutana na Mfalme Charles, ziara ya wiki hii ni ziara ya kwanza ya kifalme kwa kiongozi wa Nigeria kuelekea Uingereza kwa miaka 37.

Ziara ya mwisho ya kifalme nchini Uingereza ilifanywa mwaka 1989 na kiongozi wa kijeshi wa wakati huo, Jenerali Ibrahim Babangida.

Hakukuwa na ziara ya kifalme ya mfalme wa Uingereza nchini Nigeria katika historia ya hivi karibuni. Hata hivyo, Malkia Elizabeth II alifanya ziara rasmi mbili — mwaka 1956 kabla ya uhuru wa Nigeria, na mwaka 2003 kwa ajili ya Mkutano wa Viongozi wa Nchi za Jumuiya ya Madola.

King Charles pia alikuwa ametembelea Nigeria mara nne alipokuwa Mwana wa Wales kabla ya kuwa mfalme, akimrithi mama yake, Malkia Elizabeth, ambaye alifariki mwaka 2022.