Abbas Araghchi, sauti ya kidiplomasia inayoiwakilisha Iran katikati ya mgogoro
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araqchi. Picha/ Maktaba. / Reuters
Abbas Araghchi, sauti ya kidiplomasia inayoiwakilisha Iran katikati ya mgogoro
Araghchi ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na mmoja wa wanadiplomasia wenye uzoefu katika eneo la Mashariki ya Kati.
24 Machi 2026

Katika vita vinavyoendelea vya Mashariki ya Kati, mara nyingi Donald Trump kupitia mtandao wake wa kijamii, na vyombo vyengine vya habari, anaujuza ulimwengu kile kinachoendelea.

Lakini kutoka upande wa Iran, mtu mmoja ameibuka na kuwa sauti ya serikali na jeshi la mapinduzi. Ni Abbas Aragchi.

Basi Abbas Araghchi ni nani?

Araghchi ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na mmoja wa wanadiplomasia wenye uzoefu katika eneo la Mashariki ya Kati.

Alizaliwa mwaka wa 1962, na yeye si mwanasiasa tu, bali pia ni mwanachama wa zamani wa Walinzi wa Mapinduzi ya Iran ambaye alipigana katika Vita vya Iran-Iraq na baadaye akawa mwanadiplomasia wa kudumu.

Hata alisoma nchini Uingereza, na kupata shahada ya uzamivu PhD katika masomo ya siasa, akizingatia jinsi utawala wa Kiislamu na demokrasia inavyoweza kufanya kazi pamoja.

Araghchi alipanda cheo na kuteuliwa kuwa Balozi wa Japan na Finland na baadaye Naibu Waziri wa Mambo ya Nje.

Alikuwa mpatanishi mkuu katika makubaliano ya nyuklia ya Iran ya 2015 na mataifa makubwa ya dunia ikiwa ni pamoja na Marekani, Uingereza na EU.

Mkataba huo ulimfanya kuwa mmoja wa wanadiplomasia wanaotambulika zaidi wa Iran duniani kote.

Mnamo 2024, aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, nafasi ambayo anaitumikia mpaka sasa na kupitia nafasi hiyo, amekuwa sauti kuu ya Iran ulimwenguni.

Yuko katikati ya mivutano ya vita, mazungumzo ya nyuklia na diplomasia ya kimataifa.

Anajulikana kwa hulka yake ya utulivu lakini ya kimkakati, na uwezo mkubwa wa upatanishi.

Wakosoaji wanasema anatetea sera kali za Iran na anakosoa bila woga Marekani na washirika huku akiweka usawa wa diplomasia na vitisho.

Kutoka kwa mtaalamu wa masuala ya vita hadi mpatanishi mkuu wa nyuklia, Araghchi si mwanadiplomasia tu... ni mmoja wa wahusika wakuu wanaounda mustakabali wa Iran hivi sasa.